Featured Kitaifa

NDAISABA AIOMBA SERIKALI KUTOA SULUHU YA UMEME VIJIJINI, APONGEZA JUHUDI ZA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor
Na Mwandishi wetu _ Fichuzi  News blog
Mbunge wa Jimbo la Ngara ameibua hoja nzito kuhusu changamoto ya kukatika kwa huduma ya umeme katika baadhi ya vijiji jimboni humo, akilitaka Bunge kufahamu hatua zinazochukuliwa na TANESCO pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kurejesha huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Akichangia hoja kwenye Bajeti ya Wizara ya Nishati iliyowasilishwa bungeni hapo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, Bungeni Dodoma Mbunge wa Jimbo la Ngara Mkoani Kagera Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro ameshauri mitungi ya gesi inayosambazwa na REA iendane na majiko yanayokubali kupikia kwa kutumia umeme na gesi ikiwa ni pamoja na kuondoa makato (tozo) kwenye vifaa vya kielektroniki kama vile majiko ya gesi, brenda, tv, n.k ili wananchi wa vijijini waweze kununua vifaa hivyo kwa gharama nafuu.
“Ombi langu kwa serikali tunaomba muanze kutufungia transfoma zenye ukubwa wa KVA 100 – 200 badala ya hizi zilizopo za KVA50 Hii itasaidia wananchi wengi kuunganishwa umeme na katika kuongeza matumizi ya umeme niwaombe Wizara kufanya mchakato wa mitungi ya gesi iende sambamba na majiko yanayokubali kutumia umeme na gesi, hii itasaidia endapo mwananchi akisubiri kwenda kununua mtungi wa gesi aweze kuunganisha jiko lake na kwa kutumia umeme uliopelekwa majumbani kwani kwasasa wananchi kwa kiasi kikubwa wanatumia umeme huo kwa matumizi ya mwanga, na viwanda”, amesema Ndaisaba.
“Naomba kujua TANESCO na REA wamejipangaje kurudisha huduma ya umeme ikitokea umekatika ama miundombinu imesumbua , nina vijiji vitano ambavyo Transfoma zimeungua na wananchi wanasubiria huduma ya umeme kwa muda mrefu ambavyo ni Mkalinz, Kititiza, Mkubu, Mumilamila, na Mganza nakuomba Mheshimiwa Waziri uje na suluhu ya ni lini wananchi wangu watapata huduma wakati utakaokuja kuhitimisha hoja”, amesema Mbunge wa Ngara.
Aidha ametoa pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ajenda ya nishati safi kwani kwa kiasi kikubwa imeondoa matumizi ya vibatari katika maeneo mengi vijijini hasa katika jimbo la Ngara, pongezi hizo pia amezitoa kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dkt. Doto Biteko na wasaidizi wake kwa utendaji kazi uliotukuka.

About the author

mzalendoeditor