Featured Kitaifa

KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA YAENDELEA KUNUFAISHA WANANCHI WA MKOA WA KASKAZINI UNGUJA

Written by mzalendoeditor

Kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyoanzishwa kwa juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Wananchi wa Fujoni wamepata fursa ya kufikiwa na watoa huduma za msaada wa sheria kupitia kampeni hii, ambapo waliweza kuwasilisha changamoto zao mbalimbali kwa wataalamu wa sheria waliopo. Masuala yaliyowasilishwa yalihusu migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa na mirathi, pamoja na haki za watoto na wanawake.

Watoa huduma wa msaada wa sheria waliwasikiliza wananchi kwa makini na kuwapa ushauri wa kitaalamu, huku wakitoa elimu ya haki na taratibu za kisheria ili kuwawezesha kutatua matatizo yao kwa njia sahihi na ya amani.

Wananchi walieleza kufurahishwa na hatua hii, wakisema kuwa huduma hizi zimewasaidia kuongeza uelewa wa haki zao na namna ya kujilinda kisheria, hasa kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kupata mawakili binafsi.

Kampeni hii inalenga kuhakikisha kuwa msaada wa kisheria unawafikia wananchi wa makundi yote nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha utawala wa sheria na haki kwa wote.

About the author

mzalendoeditor