Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi kutoka Tanga, Mwanza na Pemba wameshiriki katika kikao kazi ili kuimarisha stadi za kuboresha taasisi zao kuwa vituo vya umahiri katika baadhi ya fani za ustadi zinazotolewa na vyuo hivyo.
Mafunzo hayo yanatolewa katika muktadha wa sera ya taifa ya elimu iliyoboreshwa inayosisitiza umuhimu wa elimu na ujuzi.
Akifungua mafunzo hayo Jijini Dodoma leo, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi toka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Selukele , aliwahimiza wakuu wa vyuo kuongeza ubunifu ili vyuo vyao viwe vituo vya umahiri katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi.
“Tuna hitaji kubwa kuhakikisha kuwa vyuo vyetu vinatoa mafunzo ya ufundi stadi na kutoa stadi ambazo zinahitajika katika soko la ajira la sasa na la baadaye,” amesema.
Kupitia ushirikiano na mradi Inclusive, Green and Smart Cities unaotekelezwa na shirika la ushirikiano wa kimataifa la Ubelgiji, Enabel, Serikali inaviwezesha vyuo vya VETA vya Tanga, Mwanza, FETA Mwanza, Vitongoji na Daya vya Pemba ili umahiri wake uwe wa kuigwa na vyuo vingine.
Ili kufikia malengo hayo, taasisi hizi zimeshaandaa mipango mikakati yao kila mmoja ukizingatia malengo ya taasisi husika.
“Mipango hii inazingatia ushirikiano na sekta binafsi ambao ni waajiri, matumizi ya teknolojia ya digitali, kuboresha miundombinu ya taasisi na kuzingatia ubora,” amesema Thomas Aikaruwa, Mshauri wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi wa Enabel.
Sera ya elimu iliyoboreshwa inatilia kipaumbele elimu na mafunzo ya ufundi ambayo sasa yameijumuishwa katika mtaala wa elimu tangu ya msingi hadi ya chuo kikuu.