Na. Leah Mabalwe, VIWANDANI
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Zainabu Abdallah amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 na kuushangilia katika maeneo yote utakapopita hasa katika Shule ya Sekondari Miyuji B utakapoweka jiwe la msingi shule hiyo.
Aliyasema hayo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2025.
“Nipende kuwahamasisha wananchi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 na kuukimbiza katika maeneo yote Jiji letu la Dodoma. Tunawategemea sana wananchi kwasababu Mwenge wa Uhuru ni mali yetu sote, tujitokeze na tushirikiane kuukimbiza katika maeneo yote” alisema Mwl. Abdallah.
Alisema kuwa miongoni mwa miradi itakayotembelewa ni Shule ya Sekondari Miyuji B. Mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi ujenzi wa mabweni mawili, vyumba vinne vya madarasa na matundu 10 ya vyoo, aliongeza.
Mwl. Abdallah ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mapokezi na Malazi alisema kuwa kamati yake imejipanga vizuri. “Katika maandalizi ya kupokea wageni ambao watashiriki katika kuukimbiza Mwenge wa Uhuru, tumejiandaa vizuri katika kuwapokea wageni wetu muhimu ili wapate sehemu nzuri ya kupumzika na kwaajili kupata afya nzuri ili kuukimbiza Mwenge wa Uhuru wakiwa na afya njema. Hivyo, tumejiandaa na kujipanga kikamilifu kwa ajili ya mapokezi haya” alisema Mwl. Abdallah.
Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma utapokelewa tarehe 26 Aprili, 2025 ukitokea Wilaya ya Bahi ukiongozwa na kaulimbiu inayosema “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.