Featured Kitaifa

DKT. JINGU ATOA MKONO WA PASAKA KWA WAZEE NUNGE

Written by mzalendoeditor

📌 Akagua Huduma Makazi ya Wazee Nunge – Kigamboni Dar es Salaam

📌 Asikiliza changamoto za watumishi

Na WMJJWM- Kigamboni Dar ES Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu atoa mkono wa Pasaka kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee Nunge Kigamboni Dar Es Salaam.

Akizungumza katika Makazi hayo Aprili 16, 2025 Dkt. Jingu amesema
Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini sana wazee, inawajali na ndio maana iko tayari kuwatunza na kuhakikisha maisha yao yanakuwa bora na yenye usalama.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwahudumia wazee wasiojiweza hasa katika kuwapatia huduma muhimu za malazi, chakula na huduma za Afya ili kuwaenzi kwa mchango wao kwa maendeleo ya taifa.

“Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anawapenda na kuwajali sana ndio maana mnaona huduma zote mnapatiwa kwa wakati ili kuenzi mchango wenu kwa taifa lenu mlioutoa katika sekta mbalimbali” amesema Dkt. Jingu

Akisoma taarifa ya Makazi ya Wazee Nunge Afisa Mfawidhi wa Makao hayo Jacklina Kanyamwenge amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekuwa ikitoa huduma zote muhimu kwa wazee katika Makazi hayo kila mwezi pamoja na kuboresha miundo mbinu mbalimbali iliyopo ili kuendelea kutoa huduma kwa wazee hao.

“Watumishi tunashukuru kwa kupatiwa mafunzo ya Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kuongeza weledi wa kuwahudumia Wazee wenye shida ya saikoloji, afya ya akili na wenye mahitaji maalum ya kihisia na uzee” amesema Jackilina.

Akizungumza kwa niaba ya Wazee Katibu wa Wazee hao Mzee Mussa Juma Muna ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo mkubwa kwao kwa kuhakikisha kila mmoja wao anapata mahitaji yote muhimu na kikubwa zaidi Bima za Afya ambazo zinawapa matibabu na yenye viwango vya juu.

About the author

mzalendoeditor