Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Wananchi wa kata za Buhigwe na Mwayaya wilayani Buhigwe mkoani Kigoma wameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa ujenzi wa barabara ya Buhigwe-Mwayaya pamoja na madaraja mawili ya mawe yanayounganisha kata hizo ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Barabara hiyo ya Buhigwe-Mwayaya Km 7 kwa kiwango cha changarawe pamoja na madaraja ya mto Mtunguruzi mita 12 na mto Muoga mita 6 yamejengwa ikiwa ni utekelezaji wa programu ya uondoaji vikwazo katika barabara kupitia mradi wa RISE chini TARURA unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Mkazi wa kata ya Mwayaya, Bw. Majaliwa Hussein ameishukuru serikali kwa barabara hiyo ambayo imewasaidia kusafirisha mazao yao sokoni bila shida kwani hapo awali kabla ya matengenezo barabara hiyo ilikuwa mbovu walikuwa wanazunguka kufikia huduma za kijamii.
Naye, Bw. Abeid Manga, mkazi wa kijiji cha Mwayaya amesema kuwa kabla ya matengenezo ya barabara hiyo walikuwa wakipata shida kupeleka wagonjwa, barabara ilikuwa na makorongo na mashimo lakini sasa wanaishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo kwani wanafika hospatali bila shida barabara ni nzuri mgonjwa anapata huduma na kurudi.
Pia, Bw. Benedicto Sandiwe mkazi wa kijiji cha Mwayaya ameishukuru serikali kwani barabara hiyo sasa inapitika vizuri na wananchi wanazifikia huduma za kijamii bila shida na sasa wanatumia dakika 10 kufika wilayani na kusafirisha mizigo bila shida tofauti na awali.
Kwa upande wake, Mhandisi Issack Mwita ambaye ni msimamizi wa mradi huo kutoka TARURA wilaya ya Buhigwe amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya uondoaji vikwazo katika barabara kupitia mradi wa RISE chini ya TARURA unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Amesema kuwa mradi huo umepunguza changamoto iliyokuwa inawakabili wananchi ya kuzunguka Km 20 kufuata huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe lakini baada ya kuifungua barabara hiyo sasa hivi wananchi wanatembea Km 10 tu kufuata huduma katika Halmashauri hiyo.