Featured Kitaifa

KAMPENI YA MAGEUZI YA KIFIKRA AMSHA ARI YAZINDULIWA MKOANI MARA

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWMM,Tarime -Mara

Naibu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amezindua Kampeni ya Mageuzi ya kifikra na matazamo wa kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha Maendeleo itakayotekelezwa ndani ya mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Akizungumza wakati akizindua Kampeni hiyo wilayani Tarime mkoani Mara Aprili 13, 2025 Wakili Mpanju amesema kuwa kampeni hiyo ni mahasusi kwa ajili ya kubadilisha na kugeuza fikra, mitazamo na mawazo ya wananchi ili wawe chachu na kitovu cha maendeleo ndani ya jamii wanayoishi.

“Niwahakikishie wana Tarime kupitia kampeni hii ya Amsha Ari hatutaacha kufika kata yeyote ndani ya Wilaya yenu kwakuwa Dkt. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali anayoiongoza anaamini kuwa jamii ikishirikishwa katika suala hili kutakuwa na maendeleo endelevu na jumuishi” amesema Wakili Mpanju

Wakili Amon amefafanua kuwa wananchi wakishirikishwa watakuwa mstari wa mbele kusimamia maendeleo yanayotekelezwa ndani ya jamii yao ikiwa ni sambamba na kuihifadhi miradi ya maendeleo ili iweze kudumu kwa vizazi vingi zaidi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jinsia na Wanawake Felister Mdemu ameeleza kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo ni kuwafuata wananchi huko waliko ili kuweka mizizi ya mabadiliko ya fikra katika jamii.

“Tumeamua kuwafuata viongozi wenzetu huku mliko, tukae tuzungumze ili tuwe na jamii salama yenye maendeleo endelevu”
amesema Felister

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Wakili Zakaria Mzese amesema kupitia kampeni ya Mama Samia ya msaada wa kisheria watahusika katika kampeni ya Amsha Ari Wilayani Tarime kwa kuwapa elimu wananchi hao wajue namna ya kutatua migogoro yao kwa njia ya usuluhishi badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Akitoa salamu za Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Goele ambaye ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Katiba na Sheria Pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuona umuhimu wa kuifikia Tarime kupitia kampeni ya Amsha Ari.

“Nawashukuru sana na niseme kuwa kampeni hii imekuja hapa Tarime wakati sahii, nitashiriki kikamilifu katika mikutano yote ya makundi mliyotarajia kukutana nayo” amesisitiza Mhe. Goele.

About the author

mzalendoeditor