Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA) uliofanyika leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA) uliofanyika leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mhe.Hamad Chande,akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA) uliofanyika leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma.

Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA), Fikira Ntomola,akizungumza wakati wa
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA) uliofanyika leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA) uliofanyika leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,amekiagiza Chama cha Wanawake wa Sekta ya Fedha (TAWIFA) kuwekeza kwenye teknolojia ambayo itawezesha kuwafikia wanawake wengi zaidi, ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao.
Dkt.Biteko ameyasema hayo leo Aprili 14, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama hicho ambapo amewataka wanawake kuwekeza katika teknolojia kufikisha huduma vijijini.
Aidha amesema kuwa wanawake wanatakiwa kuwekeza zaidi katika mifumo ya kidigitali ili kuendana na mabadiliko ya kidigitali.
“Naomba hapa nitoe rai kwenu kuwa, mkiwa mnaendelea kutekeleza majukumu yenu, msisahau kuhusu kuwekeza katika teknolojia. Maana Dunia ya sasa inazidi kwenda zaidi katika maisha ya kidigitali. Hii itasaidia kurahisisha biashara na kufikisha huduma kwa wepesi hususan katika maeneo ya vijijini,”amesema Dkt.Biteko
Hata hivyo amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 35 ya uchumi wa Tanzania unatokana na juhudi za wanawake ambao wanachangia asilimia 70 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake hasa katika mazao ya chakula.
“Wanawake wamejidhihirisha katika biashara, viwandani na katika huduma za kifedha kupitia utafiti uliofanywa na Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) mwa ka 2022 umeonesha wanawake ni 47% ya wafanyakazi wote wa sekta ya fedha. Pia wanashika 10% ya nafasi za kufanya maamuzi. Vile vile, 18% wakiwa wajumbe katika bodi za wakurugenzi sawa na wastani wa wanawake wawili katika kila bodi.”amesema
Pamoja na mafaniko hayo, Dkt. Biteko ametaja changamoto zinawakabili wanawake katika sekta ya fedha kuwa ni uhaba wa upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, elimu duni ya masuala ya kifedha na uchache wa nafasi za kushiriki katika maamuzi ya Sera za Fedha.
Pia amewataka wanawake nchini kuzingatia misingi ya malezi kwa watoto wao kwa kuwapa nafasi sawa watoto wa kike na wa kiume ili kukabili changamoto zinazotokana na mila, desturi utamaduni.
“ Kwa kushirikiana na wadau wengine Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua za makusudi ili kutatua changamoto zinazomkabili mwanamke na hivyo kuchochea maendeleo” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mhe. Hamad Chande amewapongeza wanawake nchini kwa kuanzisha Chama hicho kinacholenga kusaidia wanawake kiuchumi.
” Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuimarisha TAWiFA ili kuhakikisha nafasi ya mwanamke inazidi kuwa juu katika jamii pamoja na kuandaa mazingira rafiki kwa wanawake katika ukuzaji wa uchumi “amesema Mhe.Chande
Naye Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA),Bi. Fikira Ntomola amesema kuwa wanawake nchini wameendelea kujishughulisha ili kuhakikisha sekta ya fedha nchini inakuwa. Aidha, jamii inapaswa itambue uwekezaji kwa wanawake si hisani bali ni uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.
“ Tunaahidi kufikisha elimu ya fedha kwa wanawake katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuandaa mafunzo na warsha kwa lengo la kuongeza uwezo wa kusimamia masuala yao ya fedha na biashara,” amesema Bi. Ntomola.
Hata hivyo ameongeza kuwa TAWiFA imedhamiria kuleta mabadiliko chanya kuhusu ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha, aidha wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka sera na sheria zinazochochea uchumi jumuishi na uwepo wa usawa wa kijinsia kiuchumi na kijamii.
“Tumekuwa tukiwajengea uwezo wanawake wa kuendesha biashara zao kiufanisi, kukuza biashara zao na kupanua wigo wao kuhusu sekta ya fedha,” amebainisha Bi. Ntomola.
Pia amesema kuwa TAWiFA ipo tayari kushirikiana nao kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa umma, pamoja na tafiti za kuendeleza miradi ya kusaidia wanawake ili kujenga sekta ya fedha iliyo jumuishi.
TAWiFA kina jumla ya wanachama 204 na kimeendelea kuhakikisha wanawake wanashiriki katika sekta hiyo ili kuchochea maendeleo.