Featured Kitaifa

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI ZINGATIENI SHERIA, TARATIBU, KANUNI NA MIONGOZO – DKT JINGU.

Written by mzalendoeditor

Na WMJWWJ – Mtwara

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ili kuepuka kujiingiza katika migogoro isiyo ya lazima.

Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo Aprili 13, 2025 katika kikao kazi kati ya Watendaji kutoka Mashirika Yasiyo ya kiserikali ya Mkoa wa Mtwara na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika Ukumbi wa Boma mjini Mtwara ambapo amesema yapo baadhi ya Mashirika ambayo yanakiuka miongozo na kanuni za usajili wake na hivyo kujikuta yanaingia katika migogoro.

“Bila shaka kila mwakilishi wa Shirika aliyeko hapa anafahamu fika wakati wa usajili kuna miongozo na taratibu ambazo mlielekezwa kuzingatia, lakini cha kushangaza tunapowatembelea huko tunakuta mnafanya mambo tofauti kabisa” amesema Dkt Jingu.

Aidha Dkt. Jingu ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Mashirika hayo kuwa wabunifu kwa kutengeneza mipango mkakati endelevu ambayo itayasaidia kuendelea kudumu hata wakati ambapo wafadhili wataamua kusitisha mikataba kwa sababu mbalimbali.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara CPA Bahati Geuzye amesema Mkoa unatambua mchango mkubwa wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika suala zima la maendeleo na kuongeza kuwa milango iko wazi 

kwa yeyote mwenye ushauri au mapendekezo yenye maslahi mapana kwa Mkoa.

“Ndugu zangu washiriki wa kikao kazi hiki serikali ya Mkoa inatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, naomba niwaahidi kuwa tutaendelea kuwapa ushirikiano wa kila namna kadri mnavyohitaji ilimradi mzingatie sheria na kuweka mbele maslahi ya Mkoa na Taifa kwa ujumla” ameongezea Geuzye.

About the author

mzalendoeditor