Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dkt. Dorothy Gwajima amesema serikali za mitaa ni kitovu cha utekelezaji wa mikakati ya ulinzi na usalama wa mtoto iwapo jamii itatoa taarifa kwa wakati kuhusu changamoto za kifamilia ambazo ni tishio kwa ustawi wa watoto Ili wataalamu wa ustawi wa jamii kwenye ofisi hizo waweze kushirikiana na familia au jamii husika kupata ufumbuzi wa pamoja kulingana na fursa zilipo serikalini na kwa wadau wanaoshirikiana na Serikali.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Mtaani mkoani Mtwara, Dkt. Gwajima amesema, “watoto hukimbilia kuishi na kufanya kazi mitaani kutokana kukosa ufumbuzi dhidi ya changamoto zinazowakabili huku kukiwa hakuna aliyetoa taarifa serikali za mitaa kabla ya mtoto kutoroka nyumbani Ili wataalamu wa ustawi wa jamii waweze kusaidia ufumbuzi”.
Aidha, amesema, kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025 jumla ya vipindi 140 vya elimu kwa umma vimetolewa kupitia redio za jamii huku, migogoro ya ndoa 16,095 ilifanyiwa kazi na watoto 8,372 waliokolewa kutoka mitaani. Kwa wanaotoroka kupitia vyombo vya usafiri, yameanzishwa madawati ya ulinzi wa watoto katika maeneo ya usafiri katika mikoa 11.
Aidha, Sababu kuu za watoto kuingia mitaani zimetajwa kuwa ni pamoja na migogoro ya kifamilia, hali duni ya kiuchumi na ukosefu wa usawa. Hivyo, amehimiza umuhimu wa jamii kushirikiana a serikali za mitaa
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, amesema mkoa huo utaendelea kuweka mikakati endelevu ya kukabiliana na changamoto ya watoto wa mitaani, ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi na walezi ili kuimarisha malezi bora na kulinda haki za watoto kwa mujibu wa sheria. Aidha Amewasisitiza viongozi wa mkoa huo kufanya kazi Kwa ukaribu na wanachi ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali kama za malezi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema Maadhimisho hayo kitaifa ni moja ya hatua kubwa ambayo serikali imefanya Kwa ajili ya kuja na mpango mkakati madhubuti wa kuja na suluhu la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.