Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka amesema ili wanawake wawe viongozi wazuri suala la maadili halipaswi kuwa msamiati kwao bali linapaswa kuwa kitu cha msingi na kuongeza kuwa mataifa mengi yameinuka zaidi kwasababu yao na sio wanaume.
Prof. Kusiluka ameyasema hayo leo Aprili 12,2025 Jijini Dodoma wakati akihitimisha kongamano la Binti chuoni hapo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ambalo limeenda sambamba na kauli mbiu ya “Mwanamke kinara mwanga wa maendele”.
“Hapa Afrika hatuna viongozi wengi wanawake, aliyekaa muda mrefu tunayeweza kumkumbuka ni Hellen wa Liberia namkumbuka tumekuwa na mawaziri lakini sehemu zote ambapo wameongoza wanawake tumeona mafanikio mengi, hata wanaume tumepata nafasi ya kuongoza sana ila tumetumia fursa hizo kuleta madhara,”amesema.
Aidha, amesema chuo kikuu pamoja na mambo mengine ni sehemu inayotayarisha watu ambao baadae wanashika nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii na kubainisha kuwa wanao wanafunzi wengi chuoni hapo takribani 36,000 na kama 47% ya wanafunzi hao ni mabinti na wanao uwezo mkubwa katika masomo na uongozi.
“Ni wajibu wa chuo kikuu kuwatayarisha viongozi, kwahiyo mojawapo ya kazi ambayo tulikuwa tunafanya leo tumekuwa na mada kadhaa za kuwapa kwanza hamasa lakini kuwafanya wawe jasiri na kuwatia moyo kwamba wanaweza kuwa viongozi wazuri katika ngazi zote na bahati nzuri makamu wa Rais wa serikali ya wanafunzi UDOM ni binti na amekuwa akionesha ufanisi mkubwa katika uongozi,”amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi UDOM Jackline Humbaro amesema lengo la kuandaa kongamano hilo kwa mwaka 2025 ni kutambua nafasi ya uongozi kwa mabinti hasa kwenye siasa.
“Tunaona tunao viongozi wakubwa hasa ambao wapo Serikalini lakini bado mwamko wa mabinti ni mdogo kwenye masuala mazima ya uongozi, ndiyo maana tukapata msukumo wa kuandaa kongamano hili ili kuweza kuwapa nguvu lakini pia na kuwafundisha na kuwaonesha kuwa wao wanaweza wakajaribu na wakaweza kuwa viongozi wakubwa,”amesema.
Pia ameongeza kuwa kwa chuo hicho ndani ya Serikali ya wanafunzi mwamko wa mabinti kuwania nyadhifa mbalimbali bado ni mdogo japo wapo wanaofanya vizuri kwenye nafasi za kuteuliwa kwahiyo makongamano kama hayo yanaweza kuwa chachu kubwa kwao kuweza kugombea nafasi za uongozi.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Wineaster Anderson amesema ni lazima mabinti wajengewe uwezo ili waweze kuingia katika nafasi mbalimbali katika uongozi na kushika madaraka.
“Kwakuwa tunalenga 50/50 kama malengo makuu, huwezi kupeleka mabinti ambao hawajajengewa uwezo, kwahiyo kongamano la leo lilikuwa linalenga kuwakutanisha hawa mabinti, kuongea nao sisi ambao tumebahatika kwa namna moja au nyingine kupita katika zoefu mbalimbali za uongozi kwenye taasisi mbalimbali tumekuja kuwashirikisha ili waweze kuelewa nini kinahitajika ili mtu awe kiongozi bora,”amesema.