Na Alex Sonna,Dodoma
NAIBU Waziri Mkuu,Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano Mkuu wa Chama Cha Mawakili wa Serikali unatarajiwa kufanyika Aprili 14 na 15 mwaka huu Jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa leo Aprili 12,2025 jijini Dodoma na Rais wa Chama Cha Mawakili wa Serikali Deus Shayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mkutano huo.
Rais huyo amesema mkutano huo utakuwa ni jukwaa la Mawakili kupata fursa ya kujaliana mambo ya kitaaluma na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.
“Tunatarajia Naibu Waziri Mkuu,Doto Biteko kuwa mgeni rasmi ambapo pia Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wao watahudhuria mkutano huo,”amesema Rais huyo.
Amesema wanachama wa Chama hicho ni Mawakili na wanasheria wanaotoka kwenye taasisi za umma ambapo amedai kutakuwa na jukwaa la kitaaluma kujadili maslahi na maendeleo ya sekta ya Sheria na maadili kwenye Utumishi wa Umma.
“Hii itakuwa sehemu ya mafunzo na kujengeana uwezo pia utakuwa ni sehemu ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Chama chetu Septemba 22 mwaka 2022,”amesema Rais huyo.
“Nitoe rai kwa Waajiri wote kuwaruhusu wafanyakazi wao na kuwawezesha kushiriki kwani ushiriki huo ni muhimu,tathmini na mwelekeo kama walinzi wa uchumi,”amesema Rais huyo.
Amesema inawezekana zaidi ya Wanachama 2000 wanauhakika wanaweza kushiriki mkutano huo.