Featured Kitaifa

AfCFTA IHAKIKISHE INAAKISI MATARAJIO YA WANANCHI NA MALENGO YA AJENDA 2063 YA AFRIKA

Written by mzalendoeditor

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Dkt Hashil Abdallah,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Makatibu Wakuu wa Biashara wa Mkataba wa eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambao ulikuwa na lengo la kutathimini utekelezaji wa Mkataba huo unaofanyika jijini Kinshasa,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Dkt Hashil Abdallah amewashauri Makatibu Wakuu wa Biashara chini ya Mkataba wa eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) kuhakikisha wanaakisi matarajio ya wananchi na kuendana na maono mapana ya Ajenda ya 2063 ya Afrika tunayoitaka.
Dkt. Abdallah ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo ametoa agizo hilo April 11, 2025 wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Makatibu Wakuu wa Biashara wa AfCFTA ambao ulikuwa na lengo la kutathimini utekelezaji wa Mkataba huo unaofanyika jijini Kinshasa,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Aidha Dkt Abdallah amesema  Nchi Wanachama, Sekretarieti ya AfCFTA, na wataalamu waeendelee kutimiza wajibu wao thabiti katika kusukuma mbele ajenda ya AfCFTA.
Dkt. Abdallah amebainisha kuwa utekelezaji wa Mkataba huo ulioanza rasmi 1 Januari 2021, umepiga hatua kubwa, hususan katika kuhama kutoka kwenye mazungumzo hadi utekelezaji wa vitendo.
Amesema kupitishwa kwa nyaraka za Kisheria za awamu ya Pili ya majadiliano na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ya Umoja wa Afrika ni uthibitisho wa dhamira ya pamoja ya kuhakikisha AfCFTA inafanikiwa.
Dkt Abdallah pia amesema majadiliano yao katika siku chache zijazo yatakuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kukamilisha majadiliano ya maeneo ambayo hayajakamilika, kuboresha mikakati na kutoa mapendekezo thabiti kwa Waheshimiwa Mawaziri katika Mkutano wao wa 16 wa Baraza la Mawaziri.
Amesema mafanikio ya AfCFTA si tu kuhusu sera na makubaliano ya kisheria, bali yanahusu kubadilisha mazingira ya uchumi wa Bara la Afrika na Kupitia juhudi zinazolenga, kuimarisha biashara ndani ya Afrika, kukuza viwanda, kuongeza ajira, na kujenga uchumi imara.
“Sekta binafsi, wafanyabiashara wadogo na wa kati na wajasiriamali (SMEs) wanatutegemea sisi kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa mazuri na yenye fursa nyingi,”amesema Dkt Abdallah.
“Nawasihi tuwe na mijadala yenye uwazi, suluhisho madhubuti, na mazungumzo yenye tija. Tuhakikishe kwamba maamuzi tunayofanya ni ya vitendo, ya kuangalia mbele, na yanayoweza kutekelezeka,” amesema Dkt.Abdallah

About the author

mzalendoeditor