*Asema kiwanda cha Mkulazi kimeanza kazi na tani 19,124 zimezalishwa 2024
*Ajira zaidi ya milioni nane zimezalishwa kipindi cha Nov. 2020 hadi Febr. 2025
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na sukari inayotesheleza mahitaji ya wananchi kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi.
“Tayari kiwanda hicho kimeshazalisha tani 19,124 za sukari ya majumbani tangu kuanza rasmi uzalishaji Julai 2024 na kimetoa ajira rasmi 2,172 na zisizo rasmi zaidi ya 8,000. Kiwanda hicho, kilichozinduliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 7 Agosti 2024 kina uwezo wa kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka.”
Aliyasema hayo juzi (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.
Alisema katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vya mazao ya kimkakati; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi.
Pia, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea na utafutaji wa masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini; kuhamasisha uzalishaji unaozingatia viwango vya kimataifa; kuongeza uwezo wa mifumo ya masoko nchini ikiwa ni pamoja mfumo wa stakabadhi za ghala na kutumia fursa za diplomasia ya uchumi kupata masoko katika nchi mbalimbali.
Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Hatua hizo ni pamoja na kufanya maboresho ya Sheria 12 kupitia Sheria za Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 ya mwaka 2024 na kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji.
“Serikali pia imeanza maandalizi ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini unaolenga kuvutia uwekezaji wa nje na ndani, kuongeza fursa za ajira, uboreshaji wa miundombinu, upatikanaji wa soko la Kimataifa kwa bidhaa za ndani na kukuza ushindaji na ubora wa bidhaa.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kupanua wigo wa uzalishaji wa ajira nchini. “Kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Februari, 2025 jumla ya ajira 8,084,204 zimezalishwa katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Vilevile, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzalisha fursa za ajira nchini kupitia uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.