Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ujumbe wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Uchumi wa Taifa, Biashara na Kazi kutoka Bunge la Taifa la Zambia umewasili nchini Tanzania kwa ziara ya mafunzo ya kikazi, yenye lengo la kujifunza mbinu na mifumo bora ya usimamizi na uendeshaji wa Sekta ya Madini, sekta ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania katika miaka ya hivi karibu.
Tanzania imekuwa kivutio kwa mataifa mbalimbali kusini mwa Jangwa la Sahara, kutokana na mageuzi makubwa yanayofanywa katika sekta hiyo chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mageuzi hayo yamelenga kuimarisha utawala bora wa rasilimali madini, kuwajengea uwezo wachimbaji wa ndani, na kuvutia wawekezaji wa kimataifa kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.
Baada ya kuwasili nchini na Kupokelewa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde Aprili 9, 2025, Ujumbe huo leo Aprili 10 2025 ulipata nafasi ya kusikiliza wasilisho kutoka Tume ya Madini kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini hapa nchini pamoja na vituo vya ununuzi wa madini.
Awali akizungumza Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Ushirikishwaji wa Watanzania (local content) pamoja Wajibu wa Kampuni kwa Jamii inayozunguka miradi (CSR) Terence Ngole ameeleza kamati hiyo kuwa Tanzania imeanzisha masoko ya madini 43 na vituo vya ununuzi zaidi ya 109 nchi nzima na kwamba uanzishwaji wa masoko hayo umechangia kuondoa tatizo la utoroshaji wa madini, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi, na kuwapa wachimbaji uhakika wa bei nzuri na soko la uhakika kwa madini yao.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe wa Bunge la Zambia, Mhe. Bi. Sibeso Kakoma Sefulo, amesema kuwa Zambia ilichagua kuja kujifunza kutoka Tanzania kutokana na mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyapata katika uboreshaji wa sekta ya madini.
Amesema kuwa mfumo wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini umewavutia sana na ni moja kati ya vitu watakavyochukua na kwenda kuishauri Serikali ya Zambia kwa kuwa kimeleta manufaa makubwa Tanzania.