Na Gideon Gregory, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Machi, 2025, Serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 13.17 kwa vyama vya siasa vyenye sifa ya kupata ruzuku.
Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo Aprili 9,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya bajeti ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kusema kuwa hatua hiyo, imeendelea kusaidia kuimarisha na kuendeleza uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa nchini.
“Sambamba na hilo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia Baraza la Vyama vya Siasa imetoa mafunzo kwa viongozi na watendaji wa vyama vya Siasa ili kukuza uelewa juu ya uendeshaji wa shughuli za vyama,”amesema.
Awali akiongelea hali ya siasa nchini amesema imeendelea kuimarika kutokana na maboresho ya mifumo na jitihada mbalimbali za makusudi zinazofanywa na Serikali.
“Moja ya jitihada hizo ni marekebisho ya
sheria mbalimbali kwa lengo la kuimarisha utawala wa demokrasia hapa nchini, aidha, Mhe. Naibu Spika Bunge lako tukufu lilitunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024; Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 2 ya Mwaka 2024 na kufanya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali tayari imeshakamilisha utungaji wa Kanuni
za Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
“Kadhalika, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa kuratibu na kusimamia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura,”amesema.
Pia, ameongeza kuwa hadi Machi, 2025 uboreshaji awamu ya kwanza umekamilika katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar na maandalizi ya awamu ya Pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura yanaendelea.
“Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kuhakiki taarifa zao kwenye daftari kabla kuhitimishwa kwa awamu ya pili ya uboreshaji,”amesema.