Featured Kitaifa

BARRICK YASHAURI WANAFUNZI KUWA NA BIDII NA UBUNIFU KATIKA KONGAMANO LA AIESEC CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Written by mzalendoeditor
Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi kutoka Mgodi wa Barrick North Mara, Elibramack Joel, akiongea na wanafunzi
Wanafunzi wakifuatilia mada mbalimbali
Vijana wasomi nchini waliopo vyuoni wametakiwa kuongeza bidii, maarifa katika masomo yao na kuwa wabunifu ili kuweza kupenya kwenye soko la ajira kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo migodini sambamba na kuweza kujiajiri kwa kutumia taaluma zao pindi wamalizapo masomo.
 
Ushauri huo umetolewa na , Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi kutoka Mgodi wa Barrick North Mara, Elibramack Joel, wakati akieleza shughuli za kampuni na program zake wezeshi kwa jamii kwa Wanafunzi wa vyuo vikuu katika kongamano lililoandaliwa na taasisi ya kuchipua na kuendeleza vipaji kwa vijana ya AIESEC Tanzania ambalo limedhaminiwa na Barrick nchini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ambalo limefanyika katika ukumbi wa Nkurumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Amesema Barrick nchini ambayo inaendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals, itaendelea kutafuta rasilimali watu kwa ajili ya kufanya kazi kwenye migodi yake ikiwemo vijana wanaohitimu kutoka kwenye vyuo vikuu mbalimbali na vya ufundi vya kati hapa nchini na lengo kubwa kuhakikisha inaendelea kuibua vipaji na kupunguza tatizo la ajira hapa nchini.
 
“Ni muhimu kwa vijana wasomi kukuza utamaduni kwa kushirikiana na kuwasiliana (networking) katika juhudi za kusaka ajira ili kuleta matokeo Chanya kwenye jamii,” ameongeza.
 
Bw Joel alifafanua kwamba migodi inayomilikiwa na Barrick inatoa fursa kwa vijana wa vyuo vikuu kuomba ajira mara tu wanapomaliza masomo na wakiwa kazini wanapata nafasi ya kujengewa uwezo na kampuni pia kampuni inayo program ya kutoa nafasi ya mafunzo kwa vitendo kwa Wanafunzi wanapokuwa bado wako vyuoni.
 
Kwa upande wake, mjumbe wa bodi ya AIESEC Tanzania, Alimiya Osman amesema kwamba mapinduzi ya teknolojia yamesukuma mabadiliko makubwa kwenye sekta ya ajira ambapo ubunifu na ujuzi kuhusu sayansi na teknolojia ni muhimu kwa vijana ili kuweza kuingia soko la ushindani wa ajira hapa nchini.
 
“Waajiri wa leo hawaangalii shahada bali wanatizama zaidi uwezo, ujuzi, maarifa na uwezo wa utatuzi wa matatizo mahali pa kazi, hivyo ndio vigezo ambavyo kwa sasa waajiri wengi wanaangalia,” amesema.
 
Vivian Nicholaus Saga (21) kutoka Chuo Kikuu Cha Ardhi, anayechukua shahada ya Sayansi ya Mazingira akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake waliohudhuria, amesema kongamano hilo linasaidia kuwajengea uwezo Wanafunzi jinsi ya kujiamini na mbinu za kufanikisha kuomba na kupata ajira kwenye sekta mbalimbali.
 
Tamasha hilo la AIESEC limehudhuriwa na watoa mada kutoka Barrick, makampuni ya kibiashara na Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na kati.
Wanafunzi wakifuatilia mada mbalimbali
Mmoja wa wanafunzi walioshiriki akiuliza swali
Wafanyakazi wa Barrick katika kongamano hilo

Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wakishiriki Kongamano la AIESEC

About the author

mzalendoeditor