Featured Michezo

JAMII YAHIMIZWA KUFANYA MAZOEZI, KUPIMA AFYA MARA KWA MARA

Written by mzalendoeditor

Watanzania wamehimizwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara pamoja na kupima afya zao ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuyagundua mapema kwa ajili ya matibabu ya haraka.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Otilia Gowelle, jijini Dodoma Aprili 6, 2025, wakati wa matembezi maalum ya kuhamasisha mazoezi ya viungo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa.

“Katika kuadhimisha Wiki ya Afya, leo tumefanya matembezi kwa ajili ya kujenga afya bora hivyo, nitoe wito kwa Watanzania tuendelee kuimarisha afya zetu kwa kufanya mazoezi, kupima na kuchunguza afya mara kwa mara,” amesema Dkt. Gowelle.

Aidha, Dkt. Gowelle amewahamasisha wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, mkoani Dodoma, ili kunufaika na huduma mbalimbali za afya ikiwemo upimaji bure na elimu ya afya inayotolewa katika maadhimisho hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya, Bw. Issa Ng’imba, amesema Wizara inaendelea kuhakikisha watumishi wa umma wanashiriki kufanya mazoezi na jamii angalau mara mbili kwa mwezi.

Akizungumza wakati wa Matembezi hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Dkt. Omary Ubuguyu, amesema kuwa katika siku zote za maadhimisho ya Wiki ya Afya, yaliyoanza Aprili 3 na yanayotarajiwa kuhitimishwa Aprili 8, 2025, wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani wataendelea kupatiwa huduma za upimaji wa afya, uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, matibabu pamoja na rufaa pale inapohitajika.

Wakizungumza kwa niaba ya wakazi wa Dodoma baadhi wananachi waliopata huduma mbalimbali viwanjani wamesifu na kupongeza uwepo wa maadhimisho hayo.

Bi. Bahati Matola na Bi. Amina Ramadhani wamesema maadhimisho haya yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu masuala ya afya, na wameahidi kuwa mabalozi wa kueneza elimu hiyo kwa jamii ili kuboresha afya ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

About the author

mzalendoeditor