Featured Kitaifa

DAS ARUSHA AFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA SEKRETARIETI YA MAADILI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Katibu Tawala Wilaya ya Arusha Jacobo Rombo amefikishwa mbele ya baraza la Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Baraza hilo lililoketi leo Machi 28,2025 Jijini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti Jaji Mstaafu Bi. Rose Teemba na Wakili wa serikali Hassan Mwayunga ambapo katika shauri hilo Bw. Rombo wakati akiwa kiongozi Wilayani Mbongwe mwaka 2023 alichukua fedha taslimu kwenye kituo cha mafuta baadala ya mafuta kama ilivyokuwa imekusudiwa.

Akitoa ushahidi mbele ya baraza hilo upande wa malamikaji Afisa uchunguzi kutoka Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma Kanda ya Ziwa Innocent Denise Shetui (52) amesema kuwa kupitia video jongefu Katibu huyo alionekana akimshinikiza muhudumu wa kituo hicho kumpatia fedha na alipoulizwa alikili kuwa sauti ni yake na alifanya hivyo kwa nia njema.

“Kupitia video iliyokuwa inasambaa kwenye mitandao ya kijamii iliyokuwa na sauti ya watu wawili ambapo sauti ya mwanaume ilisadikika ni ya Katibu Tawala na sauti nyingine ya mwanamke ambaye ilisadikika ya muhudumu wa kituo cha mafuta ambapo katika klipu hiyo mwanaume alikuwa akimtaka ampatie fedha taslimu baadala ya mafuta kwamba anahitaji fedha hizo kwaajili ya matumizi mengine,”amesema.

Amesema kupitia uchunguzi walioufanya walibaini kuwa Bw. Rombo alikuwa akichukua fedha taslimu baadala ya mafuta zaidi ya mara moja kwa nyakati tofauti.

Katika shauri hilo pia aliyekuwa Dereva wake Bw. Origin Miringa na muhudumu wa kituo hicho cha mafuta Bi. Hellena Sweka ambaye ni muhudumu wa kituo alipoulizwa na mtuhumiwa kuhusu kushinikizwa kutoa fedha baadala ya mafuta alisema hakushinikizwa kufanya hivo.

“Sababu ya kufanya hivyo ni kwamba aliniambia kuna dharura ambayo hakuna sehemu atapata fedha taslimu tofauti na kwetu ambapo sisi ni mzabuni wao,”amesema.

Akijitetea mbele ya baraza hilo Bw. Rombo (39) amekataa mashtka yote yanayomkabili na kuliomba baraza liangalie dhamira yake kwani hawezi kuchukua fedha ambazo ni kiasi cha shilingi 230,000.

“Imani ya Rais kwangu kama kijana naishukuru na kama itabainika nimetenda kosa nitakuwa nimemuangusha Rais na nitaonekana kijana wa ajabu ndani ya miezi miwili kuingia kazini nimeiibia Serikali,”amesema.

About the author

mzalendo