Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Immaculate Sware Semesi,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Immaculate Sware Semesi,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita,Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya jumla ya kaguzi 9,606 na kushughulikia malalamiko 1,483 katika eneo la kelele na mitetemo
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Immaculate Sware Semesi,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
“Uchafuzi wa mazingira ulidhibitiwa katika miradi mikubwa yenye viashiria hatarishi (Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bomba la Mafuta ( EACOP), SGR ), ambapo programu 50 za elimu na vipindi 75 vya uhamasishaji vilifanyika.”amesema Dkt. Semesi
Aidha amesema kuwa Baraza limefanikiwa kuandaa vipindi 88 vya uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na mikutano 20 ya wadau kuhusu madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki.
Vilevile, kaguzi zilifanyika katika maeneo 178 ya uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki, ambapo maeneo 57 yalikutwa na makosa na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.
“Zaidi ya Tani 150 za vifungashio visivyokidhi viwango vilikamatwa, vikataifishwa na kuteketezwa kwa mujibu wa Sheria. Hata hivyo suala la udhibiti wa vifungashio vya plastiki ni letu sote kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa hivyo hatuna budi kushirikiana kwa ajili ya kuleta matokeo chanya.”amesema Dkt. Semesi
Hata hivyo amesema kuwa vibali 781 vimetolewa kwa wafanyabiashara mbalimbali. Pia, nyaraka 1,477 za ufuatiliaji zilitolewa, ambapo 1,089 zilirejeshwa na kufanyiwa mapitio na kubaini kuwa tani 165,834 za taka hatarishi kama chuma chakavu, betri zilizotumika, magurudumu, vioo, mafuta machafu, plastiki na taka za kielektroniki zilifuatiliwa kwa mafanikio kote nchini.
Amesema katika kipindi cha miaka minne, Baraza limefanya tafiti mbalimbali na kuaandaa maandiko ya miradi.
Aidha, Baraza limeratibu utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabia nchi, kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu pamoja na mradi wa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya mazingira.
Dkt. Semesi,amesema Ajenda ya tafiti imetekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja utafiti kuhusiana na changamoto za uchafuzi wa Mto Mara, Mmomonyoko wa fukwe za maeneo ya Coco Beach, Kunduchi Beach, Mbweni JKT Beach Club na KJ742 Navy, Fukwe za Mikadi, eneo la Msuka lililopo Pemba Kaskazini; Ghuba ya Mikindani na Manispaa ya Mtwara.
” Baraza limefanya tathmini ya hali ya mazingira kwenye maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi katika milima ya Hanang, Manyara na Mamba Myamba iliyopo Wilayani Same – Kilimanjaro.”amesema