* Mashine ya 9 yakabidhiwa, yakamilisha MW 2115 – JNHPP
* Aitaka Jumuiya ya Wazazi ieleze Watanzania mafanikio ya Serikali
*Asema kuongezeka kwa mahitaji ya umeme nchini kunachochea ukuaji wa viwanda
* Atoa wito kwa Watanzania kuzingatia matumizi bora ya umeme
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya nishati imepiga hatua kubwa nchini sambamba na kuzalisha umeme wa ziada dhidi ya mahitaji ya Watanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Machi 23, 2025 jijini Arusha wakati akitoa takwimu kuhusu ongezeko la mahitaji ya umeme nchini katika Kikao cha Baraza Kuu la Wazazi Taifa.
“ Rais Samia amefanya kazi kubwa katika sekta ya nishati nchini na hivi karibuni, tulikuwa nchini Barbados kueleza mafanikio yetu katika sekta hii kwa kuwa Rais Samia amefanya jitihada kubwa sana katika ya nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Ili uchumi wa nchi yoyote duniani upatikane lazima kuwe na sekta ya nishati. Aidha, katika sekta ya nishati ili viwanda viweze kuendelea umeme unaohitajika ni asilimia 40 na katika sekta ya madini umeme unaohitajika ni asilimia 30,”
Dkt. Biteko amesema mwaka 2017 hadi 2018 mahitaji ya juu ya umeme nchini yalikuwa megawati 1045, mwaka 2018 hadi 2019 mahitaji ya juu ya umeme yalikuwa megawati 1,116 mwaka 2021 hadi 2022 megawati 1,340.7.
“ Mwaka 2022 hadi 2023 mahitaji ya juu yaliyoongezeka na kufikia megawati 1,470 na mwaka 2024 hadi kufikia sasa mwaka 2025 ni megawati 1,908 ikiwa ni sawa na megawati 262, ongezeko la mahitaji ya namna hii haliwezi kutokea kama hakuna uwekezaji katika sekta ya nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Mashine ya tisa ya mtambo wa kuzalisha umeme katika Bwawa la Julius Nyerere Machi 22, 2025 imekabidhiwa na kuunganishwa kwenye Grid ya Taifa. Amesisitiza kuwa kutokana na ongezeko hilo la megawati za umeme Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere pekee linaweza kutosheleza mahitaji ya nchi licha ya kumalizika kwa muda uzalishaji wa umeme kwa kutumia mitambo ya Songas.
“Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya nishati imefanya kazi kubwa, Rais Samia ametenda maajabu katika sekta hii na ameweza kuvutia wawekezaji wengi sana kuja kuwekeza nchini,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, amesema kuwa Jumuiya ya Wazazi nchini ina wajibu wa malezi na mazingira na kuwa nishati safi ni eneo mojawapo hivyo Wizara ya Nishati ina wajibu wa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya hiyo, sambamba na kushirikiana nayo katika kampeni zake za kupeleka ujumbe kwa jamii.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amewaasa Watanzania kuzingatia matumizi bora ya umeme kwa kuacha mazoea yanayosababisha upotevu wa umeme ikiwemo kuwashaa taa bila kuwa na matumizi nazo.
Ametolea mfano kuhusu matumizi mabaya ya umeme kupitia utafiti uliofanywa na Wakala wa Nishati wa Kimataifa (International Energy Agency) ambapo asilimia 30 ya umeme unapotea kutokana na mazoea.
Katika hatua nyingine, taasisi mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) zimewasilisha mada mbalimbali katika semina hiyo.
Pia, Wizara ya Nishati kupitia taasisi zake za TPDC, REA na TANESCO zimetoa semina kwa wajumbe wa kikao hicho kuhusu Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024 hadi 2034, Matumizi Sahihi ya Nishati Safi ya Umeme.
Ambapo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Ngeleja Mugejwa ameeleza faida mbalimbali za matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan kwa watoto wa kike ambapo kupitia matumizi ya nishati hiyo itawasaidia kupata muda mwingi wa kujisomea kuliko kuandaa na kupika chakula.