Featured Kitaifa

TANZANIA NA JAPAN KUSHIRIKIANA UKUZAJI UJUZI KWA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Na, Mwandishi Wetu – DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Tanzania itashirikiana na Japan kukuza ujuzi kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika.

Mhe. Kikwete amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Utalii wa Japan Mhe. Kenichi Ogasawara ambaye aliambatana na ujumbe kutoka nchi hiyo leo Machi 21, 2025 jijini Dodoma.

Aidha, amesema serikali ya Tanzania na Japan zimekusudia kuwajengea uwezo vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa ili wawezebkushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Exchange program hii itasaidia vijana wa Tanzania na wakufunzi kwenda kupata ujuzi wa muda mfupi Japan na wataalamu wa japan kuja nchini Tanzania kutoa mafunzo hayo,” amesema

Vile vile, ameshukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kutoa wataalamu wanasaidia kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vya juu kwa kiasi kikubwa ili kuboresha hali ya maisha ya watanzania.

Katika hatua nyingine Mhe. Ridhiwani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. DKt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua mipaka nje ya nchi ili kutoa fursa kwa watanzania nje ya nchi.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan Mhe. Kenichi Ogasawara amesema Wizara ya Ardhi ya Japan na Shirikisho la Kampuni za Japan kwa maendeleo ya Miundombinu Afrika – (JAIDA) imeandaa programu ya ushirikiano ya kuwajengea uwezo wataalam wa Tanzania katika sekta za miundombinu na ujenzi.

Ameongeza kuwa, Tanzania ni moja ya Nchi ya kipaumbele katika programu hiyo ya mashirikiano ya ukuzaji ujuzi na teknolojia kwa vijana.

About the author

mzalendoeditor