Featured Kitaifa

TIB YATAJA MAFANIKIO YAKE KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE YA UONGOZI WA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor

KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo (TIB), Bi. Lilian Mbassy akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Machi 20, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo (TIB), Bi. Lilian Mbassy akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Machi 20, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna- DODOMA

BENKI  ya Maendeleo (TIB) katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita  imesema imefanikiwa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 630.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024.

Hayo yameelezwa leo Machi 20,2025 jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo (TIB)  Bi.Lilian Mbassy ,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na Mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Bi.Mbassy amesema kuwa kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 408.3 zipo kwenye mizania ya Benki, huku mifuko tisa inayosimamiwa na Benki ikichangia uwekezaji wa Shilingi bilioni 222, uwekezaji huo ni wa miradi ya muda wa miaka 5-15 katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Bi.Mbassy amesema kuwa kupitia uwekezaji huo mkubwa zaidi ya ajira mpya 12,547 zimezalishwa kutokana na Benki kufadhili miradi ya muda wa kati na mrefu nchini.

“Tunajivunia kutekeleza malengo ya Serikali kwa kuwekeza zaidi ya Shilingi 630.3 bilioni katika miradi ya maendeleo ambazo zimezalisha zaidi ya ajira mpya 12,547,” amesema Bi.Mbassy 

Aidha amefafanua  kuwa uwekezaji huu umegusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hasa katika Shilingi 162.7 bilioni zimewekezwa kuongeza usalama wa chakula na kupunguza njaa, Shilingi 4.3 bilioni zimewekezwa kuboresha elimu kupitia miradi ya taasisi za elimu, Shilingi 22.4 bilioni zimewekezwa katika upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kupitia miradi ya mamlaka za maji.

Hata hivyo amesema kuwa uwekezaji mwengine ni Shilingi 11.5 bilioni zimewekezwa katika nishati safi na nafuu kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification Expansion Programme-TREEP), Shilingi 250.7 bilioni zimewekezwa katika ukuaji wa uchumi na ajira, ikihusisha sekta za utalii, viwanda, na usafirishaji na Shilingi 24.7 bilioni zimewekezwa kuboresha miji na makazi.

Pia amesema kuwa  TIB kama benki ya maendeleo ni taasisi ya kisera ambayo ina jukumu la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa hususani kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo

“Katika mwaka 2025 Benki vipaumbele vyake vimejikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo, pamoja na kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita.”amesema 

Amesema kuwa Benki itaendelea kukuza mtaji wa Benki kwa kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa ili kupata mikopo ya riba nafuu kwaajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo yenye athari Chanya kwa jamii na uchumi.

Kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification Expansion Programme-TREEP), Benki inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia REA, kutoa mikopo kwa wazalishaji wa nishati jadidifu wanaohudumia maeneo ya vijijini ambako umeme wa TANESCO haujafika.


Bi. Mbassy amesema kuwa Benki ya Maendeleo TIB itaendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda  (UNIDO) katika kuchochea matumizi ya ethano kama chanzo mbadala cha nishati safi na nafuu ya kupikia kupitia mradi wa ‘’waste to energy’’.

Pia, Benki itaendelea na uwekezaji kwenye mamlaka za Maji na Kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi wa Makazi bora, Elimu, Utalii , Afya na upanuzi wa Bandari Kavu.

About the author

mzalendoeditor