Featured Kitaifa

SERIKALI: TAASISI ZA FEDHA ZINGATIENI SHERIA, KANUNI NA TARATIBU

Written by mzalendoeditor
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Oscar Nchemwa, akikabidhiwa vipeperushi na Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, vyenye mada mbalimbali ikiwemo akiba, mikopo na uwekezaji ambazo zitafundishwa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Na. Josephine Majura, WF, Bunda, Mara
 
Serikali imezitaka Taasisi za Fedha nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu bila kuwaumiza wananchi kwa kuhakikisha kuwa zinatoa huduma za kifedha kwa uwazi, haki na uwajibikaji.
 
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Bw. Salum Mtelela, alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ipo mkoani Mara kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.
 
“Serikali huweka kanuni na taratibu maalumu ili kulinda wateja na kuhakikisha kuwa taasisi hizi haziwadhulumu wananchi kupitia riba kubwa, ada zisizoeleweka au mikataba mibovu”, alisema Bw. Mtelela.
 
Alizitaka Taasisi za Fedha kuepuka utoaji wa mikopo holela bila kuzingatia uwezo wa mkopaji kurejesha deni na kutumia njia za kisheria katika kudai madeni badala ya vitisho na manyanyaso.
 
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Oscar Nchemwa, aliishauri Serikali kuhakikisha inadhibiti uanzishwaji holela wa Taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wananchi bila kufuata sheria.
 
Naye Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bi. Glory Swai, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha kwa watumishi wa Halmashauri hiyo.
 
Aliishauri Wizara ya Fedha ihakikishe elimu ya fedha inatolewa kwa makundi yote nchini, lakini pia itolewe kwa watoa huduma ili watoe huduma  kwa kufuata kanuni na taratibu.
 
Akizungumzia zoezi la utoaji elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara, Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa wananchi wa mkoa huo wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo muhimu kwa ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
 
Alisema kuwa mafunzo ya elimu ya fedha mkoani humo, yalitolewa katika makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, wajasiriamali, vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi zake imemaliza zoezi la utoaji elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara na timu ya wataalamu itaelekea Mkoa wa Mwanza ambao utakua mkoa wa 16 kufikiwa na elimu ya fedha kati ya mikoa 26 ya Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Oscar Nchemwa, akikabidhiwa vipeperushi na Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, vyenye mada mbalimbali ikiwemo akiba, mikopo na uwekezaji ambazo zitafundishwa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akitoa elimu ya fedha kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, mafunzo hayo yalitolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na baadhi ya Taasisi zake.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, mafunzo hayo yalitolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na baadhi ya Taasisi zake.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Bw. Salum Mtelela, akizungumza alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Oscar Nchemwa, akizungumza alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bi. Doto Mrutu, akitoa ushuhuda wa fedha anazopata kila mwezi kwa kufanya uwekezaji katika Taasisi ya Fedha rasmi wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa Watumishi wa Halmashauri hiyo yalitolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na baadhi ya Taasisi zake, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara. 
Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bi. Glory Swai, akiishukuru Wizara ya Fedha kwa kufika kwenye Halmashauri hiyo kutoa elimu ya fedha  kwa watumishi, mafunzo hayo yalitolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na baadhi ya Taasisi zake Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yenye mada mbalimbali ikiwemo masuala ya mikopo, akiba na uwekezaji yaliyotolewa na Wizara ya Fedha Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na baadhi ya Taasisi zake Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Bunda, Mara)

About the author

mzalendoeditor