Featured Kitaifa

SERIKALI YATENGA BILIONI 6.3 MIRADI YA UTAFITI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI-DKT.NUNGU

Written by mzalendoeditor

Mkurugenzi Mkuu wa Tume  ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (COSTECH) Dkt.Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17,2025 jijini Dodoma  kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Na.Alex Sonna-DODOMA

 

KATIKA miaka ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Tume  ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu(COSTECH) kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, serikali imetenga shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi ya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa leo Machi 17,2025 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt.Amos Nungu  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema kuwa sh.milioni 600 zikielekezwa katika miradi minne ya usalama wa chakula,ikihusisha udhibiti wa magonjwa ya mazao,uboreshaji wa uhifadhi wa chakula na ubunifu wa vyakula vyenye virutubishi vya hali ya juu.

Dkt.Nungu amesema kuwa kwa kuwekeza shilingi bilioni 2.3 kupitia Samia Commercialization Fund,serikali imewapa wabunifu wa Kitanzania fursa ya kuingiza bunifu zao sokoni, hii inasaidia kuondoa changamoto ya kukosekana na dhamana ili kupata mitaji.

 “COSTECH imeanzisha na kuziwezesha kongano nane bunifu katika mikoa ya Kigoma, Geita, Mafia, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Singida na Pemba ili kusaidia sekta ya viwanda na kilimo. Miradi hii imewezeshwa kwa ufadhili wa shilingi milioni 750, kuhakikisha teknolojia bora zinatumika katika kuboresha uzalishaji wa mafuta ya mawese, dhahabu na mazao ya baharini.”amesema

Aidha  amesema kuwa usimamizi thabiti wa serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,COSTECH imefanikiwa kuandaa mifumo ya usimamizi wa tafiti kwa kutumia teknolojia za kidijitali kupitia mradi wa HEET, pamoja na kuanzisha vigoda vya utafiti katika vyuo vikuu kama SUA na NM-AIST kwa ufadhili wa shilingi bilioni 4.7.

Hata hivyo  amesema kuwa  Serikali ya awamu sita imetoa fedha na kuweka mazingira rafiki kwa wanasayansi na wabunifu wa Kitanzania. Kupitia mfumo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali ya Tanzania na nchi rafiki pamoja na taasisi za kimataifa, COSTECH imepokea shilingi bilioni 5.65 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na washirika wetu. 

 “Serikali Katika kuimarisha miundominu ya utafiti, pamoja na kutoa fedha kwa vyuo vikuu imetoa bilion 9 kuhakikisha kuwa jengo la COSTECH linafanyiwa ukarabati na kujenga jengo jipya Dodoma.”amesema Dkt.Nungu

About the author

mzalendoeditor