Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wakati alipowatembelea Ofisi kwao Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha mashirikiano baina yao ili kukuza dhana ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati alipowatembelea Viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Ofisini kwao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha mashirikiano baina yao ili kukuza dhana ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Bi Mariam Othman mara baada Waziri huyo kuwatembelea Ofisini kwao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha mashirikiano baina yao ili kukuza dhana ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa.
Baadhi ya Menejimenti ya Chama cha Wanansheria wa Tanganyika (TLS) wakimskiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene baada ya kuwatembelea Ofisini kwao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha mashirikiano baina yao ili kukuza dhana ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa
Na. Mwandishi wetu-Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Serikali kupitia Ofisi anayoisimamia imekusudia kuimarisha mashirikiano na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ili kukuza dhana ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo alipowatembelea Viongozi wa Chama hicho jijini Dar es Salaam.
“Nimekuja kuwatembelea kwa sababu niligundua kuwa kila ninapopitia majukumu yangu katika kusimamia eneo la utawala bora ninaona kuna maeneo yana uhusiano mkubwa na TLS,” amesema Mhe. Simbachawene na kufafanua kuwa kwa tafsiri nyepesi utawala bora ni utawala wa Sheria na utawala wa Sheria ni utawala bora.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya TLS SURA 307 majukumu yake yameainishwa wazi na ushirikiano kati ya TLS na Serikali yako wazi na kuongeza kuwa TLS ni chombo cha Umma na kipo kwa mujibu wa Sheria ya Bunge hivyo majukumu yake hayapaswi kujificha na yanapotokea hayapaswi kuonekana kama uanaharakati.
Ameongeza kuwa TLS ina historia ndefu, na ni chombo kilichokuwepo kabla ya uhuru lakini mpaka leo kinafanya kazi nzuri na kinashirikiana na Serikali katika maeneo mbalimbali, hivyo kutokana na ushirikiano uliopo na Serikali, akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya Utawala Bora akaona asikae nyuma badala yake awatembelee ili apate cha kujifunza katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Nina hakika kuna maeneo mengi kabisa ya kushirikiana nanyi pamoja na kuwa mna Wizara mama ambayo ni Wizara ya Katiba na Sheria lakini pia ninaona kuna umuhimu wa kushirikiana na Ofisi ya Utawala Bora kwa kuwa utawala bora ni suala mtambuka.
Amesema yako maeneo mapana ya kushirikiana ili kujenga utawala bora na utawala wa Sheria ambao utasaidia upatikanaji wa haki, kukua kwa amani na utulivu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Amesema TLS kama itatimiza wajibu wake vizuri, itaisaidia sana Serikali na umma wa Watanzania kuhakikisha wanapata huduma mbalimbali kutoka katika Serikali yao na huduma ya kisheria kutoka katika vyombo vinavyosimamia haki kwa uwazi.