Featured Kitaifa

NSSF YASHUSHA TOZO DARAJA LA KIGAMBONI JIJINI DAR ES SALAAM

Written by mzalendoeditor

MKURUGENZI wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba,akizungumza  na waandishi wa habari leo Machi 17,2025 jijini Dodoma kuhusu  mafanikio na mwelekeo ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

MKURUGENZI wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba,akizungumza  na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 17,2025 jijini Dodoma kuhusu  mafanikio na mwelekeo ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Na.Alex Sonna-DODOMA
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema umewaondolea kero wananchi wa Kigamboni ambao walikuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu viwango vya tozo walizokuwa wakilipa wanapovuka darajani la la Nyerere Kigamboni jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17,2025 jijini Dodoma kuhusu  mafanikio na mwelekeo ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,Bw. Masha Mshomba, amesema awali pikipiki na bajaji zilikuwa zikitozwa Sh.1500.  
Bw.Mshomba amesema kuwa  kwa sasa bajaji zinazovuka daraja hilo zinalipa Shilingi 500 na  Shilingi 300 zinalipwa na waendesha pikipiki.
“Wastani wa makusanyo ya mapato kwa mwezi kwenye daraja hilo yameongezeka kutoka Sh.Bilioni 1.13 kwa kipindi cha Februari 2021 hadi kufikia wastani wa Sh.Bilioni 1.89 katika kipindi cha mwezi Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 66.”amesema Bw.Mshomba

Aidha amesema kuwa wanaisubiri  Serikali kujibu ombi lao la kubadilisha sheria  za malipo ya fao la kupoteza ajira kwa waajiriwa wenye elimu ya kuanzia Diploma ili waweze kuwalipa mafao yao yote kwa mara moja.

Amesema kuwa utaratibu uliopo sasa kwa mwajiriwa anayepoteza ajira anayestahili kulipwa mafao yote ni yule mwajiriwa ambaye elimu yake haijafika Diploma.

Amesema kwamba NSSF imejiridhisha kuwa inaweza kulipa fedha yote ndani ya miezi mitatu toka mwajiriwa apoteze ajira pale atakapoomba kupata mafao yake.

“Tumeomba mabadiliko ya sheria tulivyoona tunaweza kulipa fedha yote kwa wale waajiriwa wenye elimu ya Diploma wanaopoteza ajira zao.Serikali ikikubali tutalipa yote ndani ya miezi mitatu toka mwajiriwa apoteze ajira,”amesema Mshomba.

Vilevile Mshomba amesema kuwa maboresho  yaliyofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita  yamekuwa na mchango chanya na wenye manufaa katika ukuaji wa Mfuko ambapo amesema  mwenendo mzuri wa ukuaji umechangiwa na ongezeko la asilimia 92 katika thamani ya Mfuko Katika kipindi husika.

Amesema kuwa thamani ya Mfuko imeongezeka kwa asilimia 92 kutoka TZS bilioni 4,836.73 mwezi Februari 2021 hadi kufikia TZS bilioni 9,299.39 mwezi Februari 2025.

“Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango na kukua kwa thamani ya vitegauchumi vya Mfuko. Mwenendo mzuri wa ukuaji wa Mfuko unaashiria uhimilivu na uendelevu imara wa Mfuko ya wanachama,”amesema Mshomba.

Aidha Mshomba amesema kuwa malipo ya mkupuo wa awali wa Mafao umeongezeka na kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kimeboreshwa Katika kipindi husika, Mfuko ulilipa mafao ya bilioni 3,108.89 na malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka bilioni 537.08 katika mwaka ulioishia Februari 2021 hadi kufikia bilioni 909.16 katika mwaka ulioishia Februari 2025.

“Kutokana na utendaji uliotukuka wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwajali wastaafu, Mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kwanzia mwezi Julai 2022, waliongezewa kiwango cha mkupuo kufikia asilimia 35. Uamuzi huu wa Serikali wa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kwa wanachama wa NSSF pia umezingatia uendelevu wa Mfuko wetu,”amesema Mshomba.

Pamoja na hayo Mshomba amezungumzia matarajio ya Mfuko huo ambapo amesema kwa mujibu wa mpango wa mwaka wa fedha 2024/25 ni
kuendelea kutekeleza mikakati ya ukuaji wa Mfuko ili ufikie thamani ya  trilioni 11,000.00 mwezi Juni 2026,ikiwa ni mara mbili ya thamani ya trilioni 5,068.82 iliyofikiwa mwezi Juni 2021.

Pia amesema kuendelea kubaini fursa za uwekezaji katika maeneo mapya yenye faida zaidi na salama ikijumuisha masoko ya hisa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC ili kuweka mtawanyo mzuri wa vitega uchumi.

“Tarajio lingine ni kuimarisha mifumo na matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi, kupunguza malalamiko kwa wateja, kutoa huduma bora kwa wanachama wake na kuendelea kutekeleza Mpango wa uchangaiji wa hiari wa Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi waliojiajiri,”amesema Mshomba.

About the author

mzalendoeditor