Featured Kitaifa

LAAC YATAKA DOSARI ZILIZOBAINISHWA NA CAG HALMASHAURI YA KILOLO ZITATULIWE

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kuhakikisha inaziondoa dosari zote zilizobainishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Lugalo, mkoani Iringa.

Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa kamati, Halima Mdee baada ya kamati kutembelea na kukagua ujenzi wa shule hiyo.

“Dosari zote zilizobainishwa na CAG katika utekelezaji wa mradi huu zinaondolewa na kuhakikisha miundombinu muhimu inakamilika,” amesema Mhe. Mdee.

Kamati pia imeelekeza Afisa Masuuli wa Halmashauri kuandaa taarifa yenye maelezo ya kina na mchanganuo wa matumizi ya fedha zote za mradi huo na kuiwasilisha kwa CAG kwa ajili ya uhakiki.

Aidha, kamati imeitaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kufanya tathmini ya kina na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo, huku ikichukua hatua za haraka iwapo kutabainika ukiukwaji wa sheria na taratibu.

About the author

mzalendoeditor