Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA USIMIKAJI WA MFUMO WA KIDIJITALI  NA UTATUZI WA MIGOGORO CMA

Written by mzalendo

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii Mhe. Fatma Toufiq ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kusimika mfumo wa kidijitali wa utatuzi Migogoro ya Kikazi.

Mfumo huo utasaidia kuharakisha utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya kikazi kwa wakati sambamba na kupunguza gharama za kutembea au kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma.

Mhe. Toufiq amebainisha hayo leo Machi 15, 2025 alipoambatana na wajumbe wa kamati hiyo kwa ajili ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa mfumo huo wa usimamizi wa uendeshaji wa mashauri kidijitali katika ofisi za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Jijini Dar es Salaam.

Aidha ameitaka Tume kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa umma ili wawe na uelewa wa namna mfumo huo unavyofanya kazi.

“Bado inahitajika elimu ya kutosha kwa kutumia mbinu mbalimbali, iwe kwa kutumia Radio, TV`s,vikundi vya Sanaa na mitandao ya kijamii”
alisema Mhe. Taufiq.

Pia alisisitiza kuwe na njia maalumu ya utaoji elimu na upatikanaji taarifa kwa ajili ya watumiaji wa simu za kawaida maarufu kama viswaswadu ili makundi yote yaweze kuwa na ufahamu na uelewa wa utumiaji mfumo huo na kuwe na dawati la msaada ( Desk help) kwa haraka kwa ajili ya kuwaelekeza wale wote wasiokuwa na ufahamu na mfumo wa kidijitali.

Katika hatua nyingine Mhe. Toufiq amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na kutoa Zaidi ya Bilioni moja kuanzishwa kwa mfumo huu ambao utawarahishia waajiri na waajiriwa katika utatuzi wa migogoro kupitia njia ya mtandao.

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Mhe. Usekelege Mpulla, ameipongeza kamati kwa kuendelea kutetea bajeti ya Tume bungeni na ameihakikishia kamati kutekeleza na kufanyia kazi ushauri na maagizo yote yaliyotolewa na kamati.

About the author

mzalendo