Featured Kitaifa

WAKULIMA WAASWA KUTUMIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA KUNUFAIKA NA MAZAO

Written by mzalendoeditor

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo imetoa rai kwa Wananchi kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kutunza na kuuza mazao yao kwa bei halisi na kuepuka mifumi isiyorasmi kwa kuwa haina faida kama wakitumia mifumo rasmi ambayo inawanufaisha wakulima wafanyabiashara na kujenga uchumi kwa ujumla.

Vilevile kamati hiyo imeishauri Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala kuendele kufanya tathimini na kuona umuhimu wa kuweka bei elekezi za mazao na kuendelea kutafuta masoko mapya kwa maslahi ya wakulima wafanyabiashara na Taifa kwa ujumla

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deodatus Mwanyika wakati Kamati hiyo ilipotembelea Ghala la Mboje lililopo Mkoani Shinyanga kwa lengo la kujionea na kujifunza jinsi Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unavyofanya kazi na unavyowanufaisha wakulima wa Mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), ameiahidi Kamati hiyo kuwa Wizara yake itatekeleza maagizo na mapendekzo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo na kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mafanikio makubwa kupitia mfumo huo wa stakabadhi za ghala.

Aidha, Dkt. Jafo amesema mfumo huo utaboreshwa zaidi ili Watanzania wapate fursa ya kufanikisha maendeleo yao huku akitoa mfano wa zao la Choroko ambalo hapo awali lilikuwa linauzwa kati ya 200-400 kwa kilo na sasa ni 1,300 kwa kilo na kubainisha kuwa tani takribani 800000 za mazao mbalimbali zimeuzwa kupitia mfumo huo, ambapo kiasi cha trilioni 2.9 kimepatikana na kuingia kwenye mfumo, huku halmashauri zikipata takribani bilioni 87.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala Bw. Asangye Bangu amesema kuwa ili ghala liweze kupitishwa kufanya kazi chini ya mfumo wa stakabadhi za ghala, mmiliki hupitia utaratibu mbalimbali, ikiwemo kupata elimu na cheti cha uthibitisho.

Vilevile, Mfanyabiashara au mkulima anayefikisha mazao ghalani hulipwa pesa ya usafiri, na vifungashio hatua inayosaidia kuondoa changamoto ya usafirishaji wa mazao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro wamesema kupitia Mfumo wa Stakabadhi za ghala, Mkoa huo umepata faida kadhaa, ikiwemo usalama wa mazao, ongezeko la ushindani wa soko, na ushirikiano kati ya mamlaka za mkoa, wizara na wadau wa mazao kwa lengo la kuboresha na kulinda maslahi ya mkulima.

Kwa upande wake, Mfanyabiashara Agrigator, Daudi Mpina, amesema kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri, lakini ameomba maboresho kwenye mfumo wa malipo, ambapo kwa sasa malipo huchukua saa 48 baada ya mnada, lakini ameomba muda huo upunguzwe hadi saa 24.

About the author

mzalendoeditor