NA MWANDISHI WETU, OR-TAMISEMI
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, amesema tayari Serikali imetoa Sh.Bilioni 1.8 kwa ajili kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Muleba, mkoani Kagera baada ya kukamilisha hatua za kimkataba.
Mhe. Katimba ameeleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni mwendelezo wa juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya, ambapo awali halmashauri hiyo ilipokea sh.milioni 500 zilizotumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na sasa, serikali imeongeza sh.bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine ya hospitali.
Akiwa katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI wilayani Muleba leo, Machi 14, 2025 ilihusisha pia ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya Amali inayojengwa katika kata ya Mubunda, Mhe. Katimba ameeleza kuwa mkataba wa ujenzi wa hospitali hiyo umekamilika na mkandarasi anatarajiwa kukabidhiwa eneo la ujenzi ndani ya wiki hii ili kuanza kazi.
“Ujenzi wa hospitali hii ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi. Mpaka sasa, hospitali mpya 129 zimejengwa katika halmashauri mbalimbali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI,” amesema Mhe. Katimba.
Aidha, amewataka wananchi wa Muleba kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuwaletea maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.