Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), wakikagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
- Mwenyekiti Vuma ampongeza Rais, Serikali, Wizara na WMA
- Katibu Mkuu asema maono ya Rais Samia utoaji huduma bora kwa wananchi yatafikiwa
Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma amesema kukamilika kwa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), kutaongeza morali ya watumishi katika utendaji kazi hivyo kuboresha zaidi huduma zake kwa wananchi.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari, Machi 13, 2025 baada ya Kamati hiyo kuzuru na kujionea Jengo hilo jipya la kisasa lililojengwa na kampuni ya wakandarasi wazawa ijulikanayo kama Ms. Mohammedi Builders Ltd kwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 6.1
“Ujio wa Mradi huu unaamsha ari ya kufanya kazi kwa watumishi na ubunifu zaidi, jambo ambalo tunaamini litaongeza tija kwa maana ya makusanyo ya Wakala, lakini pia miradi itaenda kuwasaidia Watanzania kulindwa vizuri dhidi ya watu wasio waaminifu ambao huwapunja wananchi kwenye vipimo mbalimbali,” amesema Mhe. Vuma.
Aidha, Mhe. Vuma ametoa pongezi kwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa jengo hilo.
Vilevile ametoa pongezi kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Menejimenti yote ya Wizara pamoja na Uongozi wa WMA kwa usimamizi mzuri uliowezesha kufanikisha ujenzi husika.
Katika hatua nyingine, Mhe. Vuma amempongeza Mkandarasi wa jengo hilo na kutoa rai kwa Serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mbalimbali ili fedha wanazolipwa ziendelee kubaki nchini na kuchangia katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Samia kuwezesha ujenzi huo, pia amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawezesha kutimiza maono yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Hashil ameiahidi Kamati ya Bunge kutimiza maelekezo waliyoyatoa, hususan yanayohusu Wizara na WMA kuutumia muda wa mwaka mmoja wa matazamio ya jengo kwa kuhakikisha dosari ndogo ndogo zitakazojitokeza zinarekebishwa.
Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika kwa jengo, Katibu Mkuu amebainisha kuwa tayari makabidhiano yalikwishafanyika na kwamba utaratibu wa kuhamisha watumishi umekwishaanza.
Ujenzi wa Jengo hilo ulianza kutekelezwa Julai 2022 ambapo imeelezwa kuwa kukamilika kwake kutaokoa matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kinalipwa kama kodi ya pango kutokana na Wakala kutumia majengo ya kukodi kwa ajili ya Ofisi yake kuu kwa muda mrefu.
Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo umesimamiwa na Mshauri Elekezi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), kukagua jengo hilo, Machi 13, 2025. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Augustine Vuma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma akizungumza na waandishi wa habari baada ya Kamati hiyo kukagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akizungumza na waandishi wa habari baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), kukagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma (mwenye shati jeupe-katikati) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mshauri Elekezi, Blasius Venance baada ya Kamati hiyo kukagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Vipimo (WMA), Prof. Eliza Mwakasangula akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipozuru na kukagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipozuru na kukagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), wakikagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma (katikati-waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati hiyo, baada ya kukagua jengo jipya la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma, Machi 13, 2025. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah.