KAIMU Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Kanali Juma Mrai,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Marchi 13, 2025 wilayani Chamwino Mkoani Dodoma wakati akitoa taarifa ya uwepo wa vyeti vya kughushi vya vijana waliohitimu mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea.
Na.Meleka Kulwa-CHAMWINO DODOMA
JESHI la Kujenga Taifa JKT limewaonya vijana au watu wanaojihusisha na utengenezaji wa vyeti feki vya uhitimu wa mafunzo yanayotolewa na JKT ili kuweza kupata nafasi kwenye kampuni na taasisi zinazohitaji vijana waliopitia mafunzo hayo
Hayo yamebainishwa leo Marchi 13, 2025 wilayani Chamwino Mkoani Dodoma na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Kanali Juma Mrai wakati akitoa taarifa ya uwepo wa vyeti vya kughushi vya vijana waliohitimu mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea.
Amesema JKT imeamua kutoa onyo hilo baada ya kubaini uwepo wa baadhi ya vijana wanatumia vyeti feki kwenda kuomba kazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye taasisi na kampuni mbalimbali kitu ambacho ni kinyume na sheria.
“JKT tuko tayari kutoa ushirikiano kwa kampuni au taasisi yoyote inayotaka kufanya uhakiki wa watu waliotumia vyeti vya JKT kama moja ya kigezo cha kupata ajira, katika taasisi na kampuni hizo,”amesema Kanali Juma Mrai.
Amesema JKT wameanza msako mkali kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo na akisisitiza kuwa watakaowabaini watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuwa wanaamini kuna stationari zinazojihusisha na vitendo hivyo na kuzitaka kuacha mara moja.
Kanali Mrai amesema JKT inatoa nafasi kwa vijana kujiunga na mafunzo hayo kila mwaka kwa vijana wa kitanzania wenye sifa ili wamalizapo mafunzo ya JKT waweze kupata cheti cha kihitimu mafunzo ya JKT
kihalali.
Katika hatua nyingine amewatahadhalisha wananchi kutotapeliwa kupitia jumbe mbalimbali zinazotumwa kwenye simu za mkononi za kuombwa pesa ili wapatiwe nafasi za kujiunga na jeshi hilo na kuongeza kuwa nafasi za mafunzo hayo zitatolewa kwa njia ya mtandao na vyombo vya Habari pekee.