Featured Kitaifa

WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI WAASWA KUWAHAMASISHA WANANCHI

Written by mzalendo
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.
Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo
ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za
mkoa wa Dar es Salaam leo Machi 07,2025.

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.
Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo
ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za
mkoa wa Dar es Salaam leo Machi 07,2025.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akifafanua jambo. 

Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia Hotuba ya kufunga mafunzo hayo

Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)
imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Mkoa
wa Dar es Salaam kuwahamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha
na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua
viongozi wao.
 
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk
wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari
kutoka halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam.
 
Mafunzo hayo ya nadharia na vitendo namna ya
kutumia vifaa vitakavyotumika kwenye zoezi hilo ni sehemu ya maandalizi ya
uboreshaji wa daftari mkoani humo ambao utaanza tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025.
 
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa
ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha
kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” amesema Jaji Mbarouk. 
 
Ameongeza kuwa Tume inatarajia kuwa baada ya
zoezi hilo kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura
halali.
 
“Jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa
moja ninyi watendaji, kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yenu
kupitia nyenzo mlizo nazo,” amesema Jaji Mbarouk.
 
Amewasisitiza kuhakikisha kuwa sambamba na
kuwahamasisha wananchi wasambaze mabango waliyopewa na Tume kwenye maeneo yao
ya kiutendaji ili wananachi wapate habari za kina kuhusu zoezi hilo.
 
“Mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume
mvisambaze mapema katika kata zote zilizopo katika halmashauri zenu na kutokea
huko yafike vituoni ili iwe rahisi kwa wapiga kura na wadau wengine kujua vituo
viko wapi,” amesema.
Jaji Mbarouk amewaasa kuwa licha ya shughuli
nyingi za kiutendaji walizonazo watendaji hao wafuatilie kwa karibu zoezi hilo
na kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa.
 
Kuhusu watumishi wa vituoni, Jaji Mbarouk
amesema “ni vyema kuwasisitiza watendaji walio chini yenu kuzingatia matumizi
ya lugha nzuri pamoja na kufanya kazi vituoni muda wote hata kama hakuna
waombaji wanajitokeza.”.
 
 Katika hatua nyingine Jaji Mbarouk amewakumbusha watedaji hao kuhusu uwepo wa mawakala
wa vyama vya siasa na kuwasisitiza kuhusu umuhimu wa kuwapa ushirikiano kwa
kuwa ni wadau muhimu.
 
“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura
hivyo wapewe ushirikiano,” amesema.

About the author

mzalendo