MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imetoa maelekezo nane kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwamo kuanzisha haraka michakato ya ununuzi inayohusu fedha za Mfuko wa Jimbo ndani ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
Maelekezo hayo yametolewa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa PPRA,Denis Simba wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa NeST kwa Wakurugenzi, Wataalamu wa TEHAMA na Maofisa Ununuzi ngazi za Mikoa na Halmashauri.
Amesema ni lazima wahakikishe mchakato huo unaanishwa kwenye maeneo ambayo fedha zake zipo na hawajaanzisha ndani ya mfumo wa NeST.
Ametaja changamoto zinazokabili serikali za mitaa ambazo PPRA inakumbana nazo kuwa ni pamoja na makisio ya bajeti yasiyohalisia na kusababisha washindi kutopatikana.
Amesema PPRA itashirikiana nao kuhakikisha hizo changamoto zinatafutiwa ufumbuzi na kwamba kwa wale wajanja wanaodhani mfumo huo hauna macho, wapo mbioni kukamilisha uimarishaji wa mfumo na kuwa suluhisho kwa kutumia Tehama.
Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023,imeanza kutumika uni 2024,ikitajwa kuwa na mafanikio mengi ikiwemo kuongeza uwazi na uwajibikaji.