Featured Kitaifa

SERIKALI MBIONI KUANZA UJENZI DARAJA LA ILEMBO MKOANI RUKWA – NAIBU WAZIRI SANGU

Written by mzalendoeditor

Serikali imesema ipo mbioni kuanza ujenzi wa daraja la Ilembo lenye urefu wa mita 60 litakalogharimu kiasi cha Shilingi Bil.1.3 hadi kukamilika kwake lililopo Kata ya Mpui, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela , Mhe. Deus Sangu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Wenyeviti, Makatibu na Mabalozi wa CCM wa Kata ya Mpui, ikiwa ni ziara yake ya kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo hilo.

Mhe.Sangu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha inajenga daraja hilo ili kusaidia wananchi kupata huduma za kijamii, kibiashara na uwekezaji katika kipindi chote cha mwaka.

Amesema kuwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na ukamilishaji wa uandaaji wa nyaraka za zabuni unatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kinachosubiriwa ni kupatikana kwa fedha ili ujenzi uanze.

” Kwa sasa tunasubiri fedha ambazo zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai, mwaka huu ili kazi hiyo ianze mara moja,’ amesema Sangu.

Amefafanua kuwa Ujenzi wa daraja hilo utachochea kukua kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Kata ya Mpui kutokana na uwepo wa daraja hilo.

Mhe.Sangu ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo itasaidia kuunganisha mawasiliano katika Kata hiyo ambayo yamekuwa yakikatika wakati wa msimu wa mvua pia na Wilaya Jirani ya Kalambo .

About the author

mzalendoeditor