Kanuni ya mbinu hii si ngumu. Tambua tatizo, kuliweka bayana, kubuni ufumbuzi, kuutekeleza, kupima matokeo, kuzalisha matokeo bora, bidhaa bora zilizotkana na utatuzi ili jamii pana ifaidi ; kuachana na ufumbuzi ambao haukuleta faida mara moja na kutafuta suluhu nyingine, kuijaribu, kupima matokeo, kupima kufaa kwa suluhu, kama ni bora kuitumia, kama haifai, kuiacha mara moja.
Je, uko tayari kubadili mwelekeo mara moja iwapo utaona suluhisho ulilopendekeza halijaleta matokeo yenye tija tarajiwa ? au utang’ang’ania kwa kuwa sababu inakupa wewe au rafiki yako faida, au ina maslahi kisiasa ? karibu katika ubunifu shirikishi na maabara mubashara.
Ubunifu unakuwa shirikishi kwa kuwa watu wanaoufanya wanashirikiana, hakuna siri ya kampuni. Tatizo linalozingatiwa linagusa maisha ya wengi. Jana washirki wa warsha iliyokuwa inatambulisha mbinu hizi walikuwa ni maofisa wa serikali, watatiti, walimu wa chuo, wavuvi, wakusanya taka ngumu, wamiliki wa hoteli, wafanyabiashara, wavuvi, vijana, wanawake, wanaume, wajasiriamali katika mnyororo wa thamani wa samaki na usafi wa mazingira.
« Kupitia dhana hii ya ubunifu shirikishi watu wa sekta mbalimbali wanakaa pamoja na kuanisha changamoto mahsusi, kuidadavua na kisha kubuni suluhisho kisha kulitekeleza. Iwapo itaonekana utekelezaji wa suluhisho hauleti matokeo tarajiwa, wanakaa pamoja na kuiboresha, suluhisho linapoendelea kuboreshwa na kuboreshwa katika mazingira halisi ya matumizi hali lifae ndipo tunapokuwa kwenye maabara mubashara, » anasema Kikolo Mwakasungula Meneja na Mradi wa INCLUCITIES ambao umeendesha mafunzo ya mbinu hii mjini Mwanza.
Wakati wa mafunzo hayo, washiriki walitembelea fukwe ya uvuvi ya Kayenze ndogo ambako kuna maabara mubashara inaendelea ikitafuta suluhisho la changamoto ya matumizi makubwa ya mafuta ya petroli katika vyombo vya uvuvi na uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi yake ziwani.
Hapo Kayenze ndogo shirika la Osobo, linafanya maabara mubashara ili kupata betri za kuendesha boti za uvuvi ili kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa na kupunguza gharama za uvuvi.
Kazi ilianza kwa kufunga betri zilizokuwa zinatumika kwenye boti za kitalii kwenye vyombo vya uvuvi. Jaribio na suluhu hii halikupata mafanikio. Hapakuwa na hewa ya ukaa na petroli haikutumika lakini betri haikuwa na nguvu ya kutosha.
« Wahandishi waliendelea na utafiti wa kupata betri na injini inayoweza kuitumia. Hadi sasa betri iliyopo inaweza kutumia masaa manne na inaweza kufanya kazi bila matengenezo yoyote kwa miezi saba, » anasema Joab Omondi toka Osobo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wavuvi Tanzania, Bwana Bakari Kadabi, alipongeza suluhisho hili. « Hii ni hatua nzuri sana ambayo nimeshuhudia boti ikienda bila kupiga kelele na bila kutumia mafuta, » alisema Bwana Kadabi.
Hata hivyo alitoa rai kuwa ipo haja ya kuendelea kuboresha betri hizo. « Kwa mfano kuna haja ya kupunguz uzito wa betri hizi toka kwenye kilogram 48 ya sasa hadi pengine chini ya kilo 20. Hii itamwezesha mvuvi kutopunguza mzigo atakaochukua kwenye boti yake wakati anapotumia betri hii katika kazi ya kuvua samaki. » aliongeza Kadabi.
Pamoja na changamoto za mnyororo wa thamani katika uvuvi washiriki wa warsha walijengewa uwezo kuangalia changamoto kwenye uondoaji na udhbiti wa taka ngumu.
Mwanza ni miongoni mwa miji inayokuwa kwa kasi nchini Tanzania. Ukuaji wa miji ni mojawapo ya changamoto kubwa za wakati wetu—hasa katika miji inayokuwa kwa kasi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kama Mwanza. Miji na maeneo ni bidhaa changamano za mienendo ya kihistoria, kijiografia, na kijamii na kiuchumi, zinazokabiliwa na changamoto za mabadiliko kutokana na ukuaji wa haraka wa miji.
Washiriki wa warsha walikuwa ni wavuvi, wafanya biashara, wafugaji samaki, maafisa uvuvi na maafisa mazingira, watengenezaji bidhaa, kampuni na vikundi vya usafi wa mazingira, taasisi za kijamii.
Mradi wa INCLU-CITIES unalenga kuwezesha kutafuta suluhu shirikishi kwa changamoto hizi za mabadiliko zinazosababishwa na ukuaji wa haraka wa miji. Kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya, Shirika la Maendeleo la Ubelgiji, Enabel, linatekeleza Mradi wa Inclucities Mwanza, Tanga na Pemba ili kukuza miji yenye kutunza mazingira na shirikishi, kuzalisha ajira mpya za kwenye uchumi rejeshi na na kukuza zilizopo.
Madhumuni ya warsha hii ya siku mbili ni kuwashirikisha washiriki katika mchakato wa uundaji wa pamoja unaolenga kuimarisha ujasiriamali katika uchumi wa mzunguko na katika sekta ya uvuvi Mwanza. Mahsusi washiriki wa warsha watazingatia changamoto kuu katika uchumi mzunguko na udhibiti taka na sekta ya uvuvi katika muktadha wa Jiji la Mwanza.
Uundaji-shirikishi ni dhana ambapo mamlaka za serikali za mitaa, wakazi, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia hufanya kazi pamoja ili kubuni namna kuendesha maeneo ya mijini ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya jamii.
Kupitia mradi wa Inclucities, Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) litaendesha jijini Mwanza Kitovu cha Ubunifu cha uchumi mzunguko katika sekta ya uvuvi, kuendesha majaribio na kuongeza teknolojia mpya.
“Utata na uwepo wa fursa na changamoto katika miji inayokua kwa kasi kama Mwanza unahalalisha matumizi ya mbinu za ubunifu shirikishi ili kuweka suluhu zinazokubaliwa na wengi,” alisema Bw. Kikolo Mwakasungula, Meneja Mradi wa INCLUCITIES.
Warsha itawapa washiriki zana, mbinu, na mifumo muhimu ya kushirikiana kuleta ufanisi unaofaa katika mazingira ya mijini kwa kutumia dhana ya ubunifu-shirikishi. Kwa kutumia na mifano ya changamotohalisi ili kuwatia moyo na kuwapa washiriki mbinu za kuanza mchakato wa uundaji ushirikiano ndani ya mradi wa INCLU-Cities.
Ubunifu-shirikishi unasisitiza ushiriki ujumuishi, ushirikiano, na umuhimu wa mawazo na ujuzi wa kila mmoja. Kwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali na wenye nafasi tofauti katika jamii na taasisi mradi wa INCLUCITIES unalenga kuchochea matumizi ya mbinu za ubunifu shirikishi kutafuta suluhu ya changamoto za jamii.
“Tunaamini kuwa suluhu za changamoto zinapaswa kubuniwa katika jamii ambayo inakabiliwa na changamoto, hata kwa kutumia rasilimali chache,” aliongeza Mwakasungula.
Mwisho wa mafunzo washiriki walianza mipango ya changamoto mahsusi ikiwamo namna ya kuzuia uchafu wa plastic kuingia ziwani, kulinda mazalia ya samaki, kuondoa chupa za plastiki kwenye mazingira na kuthibiti taka ngumu katika makazi ya watu.