OR-TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainab Katimba, amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuendelea kubuni miradi ya maendeleo itakayoziwezesha kujisimamia badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.
Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo leo Februari 24, 2025 mkoani Kigoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika kikao cha Ushauri cha Mkoa huo (RCC).
Amesisitiza kuwa, licha ya Mamlaka hizo kupokea fedha za miradi ya maendeleo kutoka Serikali Kuu, zinapaswa kujisimamia na kujiendesha zenyewe.
“Sisi Ofisi ya Rais – TAMISEMI ndio tunaotekeleza Sera ya Ugatuzi wa Mamlaka kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa, na moja ya sehemu muhimu ni Ugatuzi wa Fedha, yaani Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ziwe na uwezo wa kujisimamia na kujiendesha zenyewe,” amesema Mhe. Katimba.
Akisisitiza hilo, Mhe. Katimba amewataka Wakurugenzi wa halmashauri kuwa wabunifu kwa kuwa kazi ya mamlaka hizo si utoaji wa huduma pekee, bali pia kuchochea na kuwezesha wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto, Mhe. Thobias Andengenye, ametaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati huku akihimiza matumizi bora ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo.