Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishuhudia makabidhiano ya matrekta kati ya Wizara ya Kilimo na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Februari 22, 2025. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Frank Chonya na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohamed Omary. Wilaya ya Ruangwa imepokea Matrekta matano ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kukabidhi zana za kilimo kwenye vituo 45 vya kutolea huduma nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishuhudia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Frank Chonya akiwa ndani ya moja ya matreka matano yaliyokabidhiwa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kituo cha kutolea huduma ya zana za kilimo, kilichopo Wilayani Ruangwa. Makabidhiano hayo yamefanyia Februari 22, 2025. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mhe. Hassan Jarufu na Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ruangwa Ibrahim Ndoro (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Ruangwa, wakati wa Halfa ya kushuhudia awamu ya kwanza ya makabidhiano matreka matano kwa ajili ya kituo cha kutolea huduma za zana za kilimo, ikiwa ni mapngo wa Serikali wa kukabidhi zana za kilimo kwenye vituo 45 vya kutolea huduma nchini, Februari 22, 2025.
(PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Februari 22, 2025 ameshuhudia makabidhiano ya trekta tano kati ya Wizara ya Kilimo na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango wa Serikali wa kukabidhi zana za kilimo kwenye vituo 45 vya zana nchini.
Akizungumza wakati wa Makabidhiano hayo Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi watakaopata fursa ya kutumia matrekta hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu, kuleta tija na kutimiza malengo yaliyokusudiwa
“Tunauzoefu wa matrekta tuliyoyaleta kipindi cha nyuma, hayakudumu kwa kuwa baadhi yetu tulikuwa tunayatumia kulima kwenye visiki, hii sio sawa, yatunzeni ili yale malengo tuliyoyakusudia ya kuendeleza sekta ya kilimo yaweze kutimia”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeandaa mpango wa kuhifadhi maji yanayotiririka katika mabonde ya Mpumbe, Nanguruwe, Mnindu, na lililopo eneo la Lucas Malia ili yatumike kwa kilimo cha umwagiliaji.
Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt Hussein Mohamed Omary, amesema Ugawaji wa Matrekta hayo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima.
Amesema katika awamu hiyo ya Kwanza kwa Wilaya ya Ruangwa wamekabidhi matrekta matano, majembe matano ya kulimia, vifaa vya kuchimbia na kusafisha mashamba na kifaa cha kuvunia mazao.
Amesema Katika awamu ya kwanza ya mpango huo Wizara ya Kilimo itaanzisha vituo 45 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Lengo la Wizara ya Kilimo ni kugusa mnyororo mzima wa thamani ya mazao, na tutaendelea kutoa vifaa vingine kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija”.