Featured Kitaifa

WATANO WASHIKILIWA KWA KUFANYA BIASHARA YA UPATU MTANDAONI BILA KIBALI.

Written by mzalendoeditor

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watano, Gerald Masanya [31] Meneja wa Kampuni ya LBL    – Mbeya, mkazi wa Nsalaga, Saphina Mwamwezi [23] Sekretari, mkazi wa Ituha, Edda William [29] mkazi wa Uwanja wa Ndege wa Zamani, Yohana Mkinda [29] mkazi wa Tukuyu na Macrine Sinkala [23] mkazi wa Nsalaga kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya upatu mtandaoni bila kuwa na kibali.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata taarifa za uwepo wa kampuni iitwayo LBL MBEYA MEDIA LIMITED inayojihusisha na biashara ya upatu mtandaoni na ndipo Februari 18, 2025 lilifanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na Maafisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mbeya na Idara nyingine ambapo walifika maeneo ya Mwanjelwa Jijini Mbeya karibu na duka la nguo liitwalo VUNJA BEI zilipo ofisi za Kampuni hiyo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano akiwemo Meneja wa Kampuni hiyo.

Watuhumiwa kupitia kampuni hiyo wamekuwa wakijihusisha na biashara ya upatu mtandaoni na kueleza kuwa wamekuwa wakituma “link” maalum kwa wateja ili kujiunga mtandaoni na kisha wateja hutakiwa kulipa fedha kuanzia Tsh 50,000/= hadi Tsh 540,000/= na kutakiwa kuangalia matangazo ya “movies” mbalimbali zilizowekwa kwenye “Platform” hiyo kwa madai kwamba watapata faida baada ya kuwekeza fedha zao kwa kipindi fulani. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Kampuni ya LBL MBEYA MEDIA LIMITED imekuwa ikukusanya fedha kwa kutumia mtandao kutoka kwa wananchi pasipo kufuata taratibu zozote za kisheria.

MMOJA ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA RAFIKI YAKE.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mussa Basuka [30] mchimbaji mdogo, mkazi wa Manyanya Wilayani Chunya kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa rafiki yake aitwaye Issa Mohamed [30] aliyekuwa mchimbaji mdogo na mkazi wa Kitongoji cha Manyanya Wilayani Chunya mkoani Mbeya. 

Tukio hilo limetokea Februari 18, 2025 Kitongoji cha Manyanya, Wilaya ya Chunya baada ya mtuhumiwa Mussa Basuka [30] kumpiga ngumi kichwani aliyekuwa rafiki yake aitwaye Issa Mohamed [30] ambaye walikuwa wakiishi naye chumba kimoja.

Chanzo cha tukio hili ni mzozo uliotokea baina yao wakiwa kwenye chumba walichopanga uliotokana na ulevi wakibishania zamu ya kupika chakula cha jioni ambapo marehemu alikuwa na jukumu la kupika na mtuhumiwa alikuwa na jukumu la kuchota maji.  

JELA MIAKA 30 KWA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA.

Mahakama ya Wilaya ya Kyela imemhukumu Owen Uswege Mwambera [20] Mkazi wa matenki border kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kupatikana na kusafirisha dawa za kulevya aina ya bhangi zenye uzito wa zaidi ya kilogramu 7.

Hukumu hiyo imetolewa na Mhe. Andrew Njau – SRM na Mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi Mkaguzi Msaidizi Bihemo Dawa Mayengela Februari 17, 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela kwa mujibu wa kifungu cha 15A kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (c) cha sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya sura ya 95 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 12, 2024 baada ya kubeba dawa hizo za kulevya zenye uzito wa Kilogramu 7.06 na alikamatwa na Polisi katika eneo la geti la ushuru wa mazao maarufu Mafiga Wilayani Kyela akiwa katika harakati za kusafiri nazo kuelekea Mbeya Mjini.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wale wote wanaofikiria kufanya biashara hii ya upatu/utapeli kuacha mara moja kwani endapo wataendelea Jeshi la Polisi litawafikia popote pale walipo na kuwakamata na kuwafikisha mahakamani. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linapenda kuwasihi wananchi wafanye biashara halali za kuwapatia kipato na sio hizi haramu za dawa za kulevya, utapeli na nyinginezo. Vile vile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuwasihi wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutafuta suluhisho la changamoto/migogoro yao kwa njia ya amani ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Imetolewa na:

Kaimu Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Mbeya.

About the author

mzalendoeditor