Featured Kitaifa

TAMISEMI YAKUSUDIA KUBORESHA ZAIDI HUDUMA ZA MACHO SEKTA YA AFYA YA MSINGI

Written by mzalendo

NA OR-TAMISEMI.

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za macho katika sekta ya afya ya msingi, kwa kuhakikisha miongozo na sera zinazoongoza utoaji wa huduma hizo zinaendelea kuboreshwa kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yameelezwa leo Februari 20, 2025 jijini Dodoma na katibu Mkuu OR – TAMISEMI Adolf Ndunguru kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Idara ya Afya,Ustawi wa jamii,na Lishe Dkt. Rashidi Mfaume katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa macho imara, utakaotekelezwa katika mikoa minne ya Arusha, Singida, Tabora na Manyara.

Dkt. Mfaume amesema kutokana na eneo la afya ya macho kupewa kipaumbele cha chini, OR – TAMISEMI kwa kushirikiana na wizara ya Afya, na wadau mbalimbali imejipanga kuhakikisha huduma za macho zinajumuishwa katika mfumo wa afya ya msingi ili kuwafikia watoto wengi zaidi katika jamii.

Naye, Mkurugenzi wa huduma za uuguzi na ukunga Dkt. Ziada Sellah akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, amesema inakadiriwa kuwa wastani wa watoto nane kati ya kila watoto 10,000 wenye umri wa miaka 0 -15, wana ulemavu wa kutokuona na idadi kubwa zaidi wana upungufu wa kuona.

“Serikali itaendelea kuboresha huduma za Uzazi, Mama na Mtoto ikiwemo za uchunguzi wa macho na kutoa afua sahihi kwa watoto tangu wakiwa tumboni mwa mama zao hadi wanapofika umri wa miaka mitano, kipindi hiki ni muhimu sana kwani ndio matatizo mengi yasababishayo ulemavu wa kutokuona hutokea,” amesema Dkt. Sellah

Awali, akitoa taarifa ya mpango huo, Daktari Bingwa wa macho kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Prof. Milka Mafwiri amesema lengo la mpango huo ni kupunguza ulemavu wa kutokuona unaozuilika kwa Watoto hapa nchini kwa kujumuisha afua za afya ya macho kwa watoto katika afya ya msingi hususani kwenye huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

Kwa mujibu wa Prof. Mafwiri mpango huo unaogharimu Sh.Bilioni 4.9 na utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano katika halmashauri 16 za mikoa ya Arusha, Singida, Tabor ana Manyara.

Mpango huo uliopewa kaulimbiu ya uoni bora, Maisha bora, unakuja wakati ambao watoto milioni 1.4 duniani, wanakabiliwa na tatizo la kutoona huku nusu ya idadi hiyo wakiwa ni Watoto wanaoishi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

About the author

mzalendo