Mwenyekiti wa Mafunzo ambaye pia ni Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Ndg. Emmanuel Vuri akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Na. Mwandishi Wetu
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari; la Kudumu la Wapiga Kura wameaswa
kutekeleza majukumu waliyopewa kwa kuzingatia sheria, kanuni, maelekezo na
miongozo itakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Balozi
Omari Ramadhan Mapuri wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa
daftari mkoani Morogoro leo Machi 19, 2025.
“Mnapaswa kutekeleza majukumu mliyopewa kwa kuzingatia sheria, kanuni,
maelekezo na miongozo itakayotolewa na Tume,” amewaasa watendaji hao ambao
wamehudhuria mafunzo ya siku mbili.
Balozi Mapuri ametoa wito kwa watendaji hao kuendelea kutumia muda wao
wa ziada kusoma na kupitia maelekezo yote waliyopewa ili kuongeza uelewa zaidi
kuhusu wajibu na majukumu yao wakati wa kutekeleza zoezi lililopo mbele yao.
Akifunga mafunzo kama hayo mkoani Tanga, Mjumbe wa Tume ambaye pia ni
Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari amewataka watendaji hao kusoma katiba na
sheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Someni kwa makini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya
Uchaguzi, Kanuni za uboreshaji, Maelekezo na Miongozo yote inayotolewa na Tume
ili kazi yenu ifanyike kwa unadhifu na haki,” amesema.
Jaji Asina amewakumbusha watendaji hao juu ya wajibu wao wa kuhamasisha
wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba
itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao kwenye uchaguzi mkuu
utakoafanyika mwaka huu.
Uboreshaji wa Daftari utafanyika
mkoani Morogoro na kwenye Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya
Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga kwa siku saba kuanzia tarehe 01 hadi 07
Machi, 2025 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa saa 02:00 asubuhi na kufungwa
saa 12:00 jioni.