Featured Kitaifa

TUINUKE PAMOJA : WADAU WAKUTANA KUTENGENEZA MBINU ZA KUTOKOMEZA MILA NA DESTURI KANDAMIZI KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA, DODOMA

Written by mzalendoeditor
Na Mwandishi Wetu, Kondoa
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na shirika la Aga Khan Foundation (AKF-TZ) wamewakutanisha wadau mbalimbali kwa siku mbili kujadili juu ya namna ya kutatua changamoto zitokanazo na mila na desturi zinazokwamisha ufikiwaji wa usawa wa jinsia katika wilaya ya Kondoa vijijini, Kondoa Mji na Chemba.
Warsha hii imewakutanisha wawakilishi kutoka Serikali za mitaa, Kamati ya MTAKUWWA, viongozi wa dini, viongozi wa mila, watu mashuhuri na wawakilishi kutoka vikundi 21 kutoka kwenye hizo wilaya tatu za mkoa wa Dodoma.
Amefafanua kuwa warsha hii itatoka na mpango kazi, wa wadau kwa kushirikiana na vikundi katika jamii,  wenye mikakati na mbinu mbalimbali zitakazo endeleza mila na desturi chanya zinazowezesha kufikia usawa wa kijinsia na kutokomeza mila na desturi hasi zinazokwamisha kufikia usawa wa kijinsia katika maeneo yao wanapotoka.
Akizungumza wakati wa mahojiano, mwezeshaji wa warsha, Vera Assenga amesema kuwa warsha hii imeandaliwa kwa lengo la kuendelea kuwajengea uwezo wadau juu ya usawa wa jinsia na mila na desturi na namna zinavyoweza kuchangia katika kukuza au kuzuia usawa wa kijinsia katika jamii.
Amesema kuwa warsha hii ni mwendelezo wa utekelezaji wa afua mbalimbali za mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa katika wilaya hizi tatu kwa mwaka huu wa kwanza wa mradi; mradi huu unafadhiliwa na ubalozi wa Ireland Tanzania na unatekelezwa TGNP na AKF.
Kwa upande wake Afisa msaidizi wa Mradi huu wa Tuinuke Pamoja, Rubengo Rubengo  amesema kuwa mradi huu unalenga kuwajengea uwezo na kuwezesha kifedha vikundi vya kijamiii kuendeleza harakati zao za kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake mkoani Dodoma.
Ameeleza kuwa kupitia uwezeshwaji huo, wanavikundi wataweza kushiriki kikamilifu kutatua changamoto mbalimbali za kijinsia zilizopo katika maeneo yao ikiwemo changamoto ya ukatili wa kijinsia na changamoto nyingine zitokanazo na mila na desturi kandamizi.
Ameongezea kuwa tunategemea warsha hii itatumika kutoa msingi mzuri kwa vikundi hivyo vya kijamii kushirikiana na wadau hawa muhimu katika kutatua changamoto hizo kwa lengo la kuleta usawa wa kijinsia katika wilaya hizi za Kondoa na Chemba.

About the author

mzalendoeditor