Na.Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kukabidhi boti zaidi ya 80 kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa buluu kwenye mwambao wa bahari ya Hindi mkoani Tanga.
Rais Dkt. Samia anatarajia kukabidhi vifaa hivyo vya kisasa kwa vikundi mbalimbali vya wavuvi, pamoja na wanawake wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo cha zao la Mwani wakati wa ziara yake anayotarajia kuifanya hivi karibuni Mkoani Tanga.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian wakati wa Mahojiano maalumu kuhusu maandalizi ya Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kumokea Rais Samia, ambaye anatarajia kufanya ziara ya siku nane Mkoani Tanga, kuanzia Tarehe 23 mwezi Februari.
” Pamoja na mambo mengine ya msingi, Raisi Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajia kukabidhi boti za uvuvi pamoja na kilimo cha mwani ili kukuza uchumi wa buluu katika mkoa wa Tanga wenye urefu wa zaidi ya Kilomita 180 za bahari,” Dkt. Burian amesema.
Amesema mkoa wa Tanga unaobeba historia ya kipekee hapa nchini, umebarikiwa kuwa na fursa za kipekee za uchumi wa buluu, lakini mkoa bado haijaweza kunufaika vya kutosha kupitia fursa hiyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kisasa.
” Ni matumaini yangu kuwa, msaada ambao Raisi Dkt Samia anatarajia kutoa utaleta changamoto chanya ya kuuwezesha Mkoa wetu kunufaika vya kutosha kupitia uchumi wa buluu,” alisema.
Pamoja na hayo, Dkt Burian aliongeza kuwa, Raisi Dkt Samia pia anatarajia kutoa zaidi ya mitungi 20,000 ya Gesi kwa ajili ya kuongeza kasi ya kampeni ya matumizi ya nishati salama, na kupiga vita dhidi ya uchafuzi wa mazingira Mkoani Tanga.
“Tanga tunamshukuru sana Mh. Raisi Dkt Samia kwa ajili ya kutupa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi muhimu ya kiuchumi na kijamii, ametufanyia mengi sana tangu aingie madarakani, na kupitia ziara yake hii, tunatarajia kunufaika zaidi,” alishukuru.
Akieleza juu ya Maandalizi ya ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa, Balozi Burian amesema maandalizi yanaendelea vizuri.
“Maandalizi ni makubwa sana, kwa kiasi kwamba tunatamani akija tumvalishe mavazi ya asili ya Tanga, na kumnywesha Uji wa asili,” Akieleza kwa furaha.
Amesema miongoni mwa miradi atakayo tembelea ni pamoja na Bandari ya Tanga, mradi wa umwagiliaji, shule ya mchepuo wa sayansi kwa wasichana na kuweka mawe ya msingi katika Bomba la Mafuta.