Featured Kitaifa

DARAJA LA MTO KALAMBO LAWANUFAISHA WANANCHI MKOANI RUKWA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu Kalambo, Rukwa

Imeelezwa kuwa ujenzi wa daraja la mawe la mto Kalambo lenye urefu wa mita 60 linalounganisha vijiji vya Mkowe, Mao na Katapulo katika kata ya Mkowe halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuwa limerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Diwani wa kata ya Mkowe, Mhe. Alfred Mpandashalo ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea daraja hilo ambalo limekuwa mkombozi kwa wananchi wa vijiji vya Mkowe, Katapulo na Mao hadi kufika makao makuu ya wilaya kufuata huduma za kijamii.

“Daraja hili linatoka kata yetu ya Mkowe kuelekea kata ya Mpuluma, kabla ya ujenzi kipindi cha masika maji yalikuwa yakijaa sana, tumepoteza ndugu zetu waliofariki kwa kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka mto huu, hata mifugo yetu pia ilikufa, lakini sasa baada ya daraja hili wananchi wamefurahi kwani linatusaidia kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi”, alisema.

Naye, Bw. Joseph Chakupewa, mkazi wa Kijiji cha Mkowe, ameishukuru serikali kupitia TARURA kwa kuwajengea daraja hilo kwani hapo awali wanafunzi, wajawazito na hata wakulima walipata shida kuvuka kufuata huduma za kijamii, lakini sasa daraja hilo limekuwa mkombozi kwa wananchi katika shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wake, Mhandisi Collins Mlashani, msimamizi wa mradi kutoka TARURA wilaya ya Kalambo, amesema daraja la mto Kalambo lililopo barabara ya Kanyalakata-Mao-Mkowe yenye urefu wa Km 27.6 limejengwa kwa kutumia mawe kupitia mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo chini ya mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ambapo ameeleza mpaka sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 95.

Ameeleza kuwa kazi zilizobaki ni kunyanyua tuta na kuweka alama za barabarani ambapo ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha ili kuweza kuwasaidia wananchi kufikia huduma za kijamii na kurahishisha mawasiliano.

About the author

mzalendo