Featured Kitaifa

WANANCHI WA PASUA NA MAJENGO WAFURAHIA FURSA ZA UWEKEZAJI

Written by mzalendoeditor
Mchambuzi Fedha Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Gladness Mollel akitoa elimu ya fedha juu ya Uwekezaji katika Hati Fungani wakati wa semina ya  Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Kata ya Majengo Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Na. Eva Ngowi, WF, KILIMANJARO
Serikali imetoa rai kwa Wananchi kuwekeza fedha zao sehemu sahihi na salama badala ya kuwekeza fedha mahali ambapo pana vihatarishi.
Rai hiyo imetolewa katika Semina ya Elimu ya Fedha iliyotolewa katika Kata za Pasua na Majengo, Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Akiongea katika semina na Wajasiriamali wadogo, Vyama vya Waendesha Boda Boda/Bajaji na Vikundi vya Vikoba, Mchambuzi Fedha Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Gladness Mollel alisema kuwa ni vyema wananchi wakawekeza kwenye Masoko ya Mitaji ikiwemo uwekezaji katika Hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa, Hati Fungani za Serikali na za Kampuni na katika Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja.
“Kuna faida nyingi za kuwekeza katika Hisa ikiwemo kupata gawio, ongezeko la thamani linalotokana na kupanda kwa thamani ya hisa” Alisema CPA Mollel
Alifafanua kuwa Hati Fungani za Serikali hutolewa kwa Umma na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa niaba ya Serikali kupitia Soko la Awali ili kuiwezesha Serikali kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na kwamba CMSA huidhinisha utoaji wa hatifungani za kampuni ili kuziwezesha kupata mitaji na kutekeleza majukumu yake yaliyopangwa.
“Baada ya mauzo ya awali, Hati Fungani huorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambapo huuzwa na kununuliwa na wawekezaji mbalimbali kulingana na nguvu ya Soko.
Uwekezaji katika Hati Fungani unamsaidia mwekezaji kupata riba ya kila mwaka waliyokubaliana awali hadi pale Hati Fungani hiyo itakapokomaa. Vilevile, Mwekezaji anaweza kutumia hatifungani kama dhamana ya mkopo na huweza kukopeshwa na Benki za Biashara.” Alifafanua CPA Mollel.
Aidha, CPA Mollel alisema kuwa Uwekezaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja unahusisha kununua vipande kutoka kwa Meneja wa Mfuko ambapo mwekezaji ataweza kupata faida pale ambapo bei ya kipande inapoongezeka.
“Nawashauri wananchi kuwekeza kwenye Masoko ya Mitaji na Dhamana kwani ni salama kwa sababu hakuna athari.” Alisema CPA Mollel.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano, kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga alisema kuwekeza kwenye Taasisi zilizosajiliwa kwa Mujibu wa Sheria inawezesha mwananchi kuwa na uhakika wa usalama wa mitaji yao, kupata faida shindani na kuwa na uhakika wa ukwasi endapo watahitaji tena kupata fedha zao.
”Tumepata fursa ya kukutana na wajasiriamali hapa Pasua na Majengo, na kuwapa elimu ya fedha kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo kuwekeza kwenye Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja inayoendeshwa na UTT AMIS. Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja inawawezesha wananchi wengi zaidi kuendeleza utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza kwa urahisi kwenye Masoko ya Fedha na Mitaji kama sehemu mbadala ya uwekezaji.
“UTT AMIS tunaendelea kusisitiza kuwa pamoja na mambo mengine, kuwekeza katika Mifuko sahihi ni uwekezaji ambao utawasaidia mbali na shughuli zao za biashara wanakuwa na uhakika wa kupata kipato nje ya biashara ile wanayoifanya moja kwa moja” Alisema Bw. Mwanga
Aidha, Bw. Mwanga alifafanua kuwa kupitia Mifuko ya Umoja, Wekeza Maisha, Watoto , Kujikimu, Ukwasi na Hati Fungani wananchi wanaweza kuanza kuwekeza kwa kiasi cha chini cha shilingi 10,000 hadi 100,000 kutegemeana na aina Mifuko.
Akitoa Elimu kwa Wananchi Bw. Rahim Mwanga aliongeza kuwa, Wawekezaji wanapata faida nzuri na shindani kati ya asimilia 12 hadi 15 kwa mwaka kulingana na hali ya soko. Pia urahisi wa kuwekeza na kutoa pesa. Wawekezaji wanaweza kujiunga kwa kupiga msimbo *150*82# na kuwekeza kwa kupitia mitandao yote ya simu na benki zote nchini.
Diwani wa Kata ya Majengo Mhe. Humphrey Nelson Mosha akisoma vipeperushi ya Elimu ya Fedha alivyopewa wakati wa Semina ya Elimu ya Fedha kuhusu uwekezaji iliyofanyika katika Kata ya Majengo Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Mchambuzi Fedha Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Gladness Mollel akitoa elimu ya fedha juu ya Uwekezaji katika Hati Fungani wakati wa semina ya  Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Kata ya Majengo Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano, kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akitoa elimu ya fedha kuhusu Uwekezaji unaopatikana UTT AMIS wakati wa semina ya  Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Kata ya Majengo Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Afisa Mkuu Mwanadamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, akitoa Elimu ya Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo, waendesha BodaBoda na Vikundi vya Vikoba katika Kata ya Pasua Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
Afisa Usimamizi Fedha Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bw. Jackson Mshumba, akitoa Elimu ya Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo, waendesha BodaBoda na Vikundi vya Vikoba katika Kata ya Pasua, Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoani Kilimanjaro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF- Kilimanjaro)

About the author

mzalendoeditor