*▪️Asisitiza Serikali itaendelea kuwawezesha wawekezaji wazawa*
*▪️Aeleza mpango wa Serikali wa kukabiliana na ugonjwa wa Malaria nchini*
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wakala wa Brabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ihakilishe inatoa kandarasi za ujenzi na ukarabati wa barabara kwa wakandarasi wenye uwezo wa kujenga kwa viwango vinavyoendana na thamani ya fedha.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 13, 2025) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbasi Tarimba aliyehoji kwanini Serikali isianze kutumia vikosi kazi vya Manispaa au TARURA badala ya wakandarasi binafsi katika ukarabati wa barabara zilizoharibika, katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, bungeni jijini Dodoma.
“Tunaitaka TARURA iwasimamie wakandarasi binafsi wanapopewa kazi, wawe na uwezo wa kujenga barabara za kudumu kwa mujibu wa viwango vilivyopo ili barabara ziweze kutumika kwa muda mrefu. ”
Amesema kuwa awali mfumo wa ujenzi wa barabara za vijijini uliokuwa unaruhusu Halmashauri kukarabati barabara zake ulibaini kuwa na mapungufu hasa kutokana na uwezo tofauti wa kifedha wa baadhi ya Halmashauri.
“Serikali iliwasikiliza waheshimiwa Wabunge ambao wakati wote mlipokuwa mnaomba baadhi ya barabara zenu kwenye Halmashauri zihamishiwe TANROADS, kutokana na maombi ya mara kwa mara tuliamua kuunda TARURA inayoshughulikia barabara za vijijini na mijini na inafanya vizuri. ”
Kadhalika Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa TARURA kwa ajili ya matengenezo ya muda mfupi. “TARURA tumieni fedha hii vizuri ili kufanya ukarabati kwenye barabara zenye uhitaji wa kukarabatiwa ili ziendelee kutumika. ”
Wakati huohuo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya udhibiti wa ugonjwa wa Malaria ikiwemo uendeshaji wa kampeni ya usafi ambayo inagusa pia maeneo yenye mazalia ya mbu. “Pia tunaendelea na utoaji wa neti kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania kujikinga na Malaria”.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa hamasa kwa wawekezaji kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za kutibu ugonjwa malaria na za kupuliza jwenye mazalia ya vijidudu vya Malaria.
“Wengi mnafahamu kuwa pale Kibaha mkoani Pwani tunacho kiwanda cha kutengeneza dawa za kunyunyiza kwenye mazalia ya mbu, Halmashauri sasa zinapaswa kutenga fedha ili kwenda kununua dawa na kunyunyiza kwenye maeneo yote yenye mazalia ya mbu. ”
Akijibu Swali la Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwalinda na kujenga ushindani wa wawekezaji wazawa, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imetengengeza mazingira nafuu ya uwekezaji kwa wazawa kwa kupunguza kiwango cha uwekezaji kutoka Dola laki moja hadi dola elfu hamsini.
“Tumeendelea pia kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa wazawa ikiwemo kupunguza kiwango cha kodi kwa bidhaa zinazozalishwa ndani na hata mchakato wa upataji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji. ”