*đź“Ś Mitungi 3,255 yaanza kusambazwa wilayani Mbozi*
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited, tarehe 12 Februari, 2025 imeanza rasmi kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa wakazi wa mkoa wa Songwe na Wananchi wa wilaya ya Mbozi wameanza kununua mitungi hiyo kwa nusu bei.
Mkuu wa mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo amewapongeza REA pamoja na kampuni ya Oryx kwa kuanza kugawa mitungi hiyo katika muda muhafaka na kutoa wito kwa REA na Oryx kuendelea kutoa elimu kuhusu usalama wa gesi ya kupikia (LPG); faida ya nishati safi na salama kiafya na namna zinavyochangia katika utunzaji na uhifadhi mazingira.
“Mpango huu wa kusambaza mitungi ya gesi ni mzuri na kama mnavyofahamu; Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mama Samia Suluhu Hassan ni Mhamasishaji namba moja wa nishati safi siyo tu barani Afrika bali Duniani kote, kwa ujumla na sisi tunaoishi mikoa ya pembezoni, ndiyo waathirika wakubwa wa changamoto, zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.”
“Naipongeza REA kwa kuanza kutekeleza Mradi huu, nawapongeza pia Oryx kwa kwa kuwa sehemu ya ajenda ya kusambaza nishati safi kwa Watanzani. Huu ni uzalendo wa hali ya juu kwa Taifa letu”. Amesema Mhe. Chongolo, Mkuu wa mkoa wa Songwe.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Nishati Safi mkoa wa Songwe kutoka REA; Bwana Vencha Maganga amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya kusambaza nishati safi ikiwemo gesi ya kupikia (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji na kuwaomba Wananchi wa mkoa wa Songwe kuchangamkia fursa ya kununua mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ambayo ni shilingi 20,000 tu na fedha inayobaki, inalipwa na Serikali.
“Lengo letu ni kutoa elimu na kuwawezesha Wamama ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa nishati chafu ili wapate nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi. Nawaomba Wananchi wafike kwenye vituo vya kuuzia mitungi hiyo, wakiwa na Vitambulisho vya NIDA kwa ajili kununua mitungi hii, pamoja na vifaa vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi (20,000/=) tofauti na ambavyo wangenunua kwa shilingi (40,000) na kuendelea”. Amekaririwa, Bwana Maganga.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi; Mhe. George Msyani amewapongeza Wananchi kufika kwenye kituo cha mauzo ili kununua mitungi hiyo kwa bei ya ruzuku katika kitongoji cha Mlowo, wilayani Mbozi.
Wilaya zitakazonufaika na usambazaji wa mitungi hiyo ya gesi kwa mkoa wa Songwe ni pamoja Mbozi, Ileje, Momba na Songwe