Featured Kitaifa

RC KILIMANJARO AWAASA WANANCHI WA KILIMANJARO KUACHA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA

Written by mzalendoeditor
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw, Nurdin Babu akizungumza na Timu ya Wataalam wa kutoa Elimu ya Fedha, Kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi zake ofisni kwake kabla ya kuanza zoezi la kutoa Elimu ya Fedha katika Wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro
Na. Eva Ngowi na Chedaiwe Msuya, WF, KILIMANJARO
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Nurdin Babu amewaasa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuacha matumizi mabaya ya fedha , huku wengine wakiwa na mitambo ya kuiibia Serikali na wananchi.
Bw. Nurdin Babu ametoa maagizo hayo wakati wa kikao na Waandishi wa Habari na Timu ya Wataalamu ya utoaji wa Elimu ya Fedha, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iliyofanyika Wilaya ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kupitia elimu hiyo ambayo itawafikia makundi mbalimbali itasaidia wananchi kutambua matumizi sahihi ya fedha. Pia nimefurahi kusikia mtafika katika Shule za Msingi na Sekondari; mtawasaidia vijana kwa sababu wapo vijana hawatambui thamani ya fedha” Alisema Bw. Nurdin Babu
Aidha Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Yusuphu Nzowa m, alisema anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuleta Timu ya Wataalamu ya utoaji wa Elimu ya Fedha kwa Mkoa wa Kilimanjaro kwani itawafikia wananchi hasa wastaafu ambao baada ya kustaafu wanajikuta wameingia kwenye biashara ambazo hawana taaluma nazo na kuwasababishia hasara.
“Nashukuru kwa ujio huu kuja kutoa Elimu hii kwani itawafikia wananchi hasa wastaafu, kwani kumekuwa na kasumba ya wastaafu wengi kujiingiza katika biashara ambazo hawana taaluma nazo baada ya kustaafu hivyo kuwapelekea kupata hasara kubwa.” Alisema Bw. Nzowa.
Awali akizungumzia madhumuni ya Elimu ya Fedha, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionensia Mjema alisema; Serikali inataka kuweka uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa nchini ili kujenga uchumi na kuondoa umasikini, Kuinarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia Elimu ya Fedha, kuongeza upatikanaji wa Huduma za Fedha, Kutoa elimu ya kuwezesha kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha, kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha, kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao, kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na kulipa madeni; na kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Fedha kwenye ukuaji wa Uchumi.
Bi. Mjema alisema kuwa Timu ya Wataalamu ya utoaji wa Elimu ya Fedha kwa Mkoa wa Kilimanjaro imelenga kuwafikia wadau mbalimbali wakiwemo; wahamasishaji wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Vikundi vya kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha, Watoa Huduma za Fedha, Vikundi vya wanawake, Vijana na Watu wenye Mahitaji Maalum, Vikundi vya Boda boda, Machinga, Wafanyabiashara, Wakulima, Watumishi wa Umma, Wanafunzi, Wakufunzi, Wajasiriamali wadogo na wa kati, Asasi za Kiraia, Wahariri na Waandishi wa Vyombo vya Habari, Watoto na Umma kwa ujumla.  
Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, Elimu hiyo itatolewa kwa siku kumi na nne (14) katika Wilaya za Moshi Manispaa, Moshi Vijijini, Rombo, Same, Mwanga na Hai.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Nurdin Babu (aliyevaa Kaunda suti ya Dark Blue) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalam wa kutoa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi zake, ambao watatoa elimu hiyo kwa siku kumi na nne (14) kwa Wilaya sita za Mkoa wa Kilimanjaro.
Katibu Tawala Mkoa Wa Kilimanjaro, Bw. Yusuphu Nzowa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalam wa kutoa Elimu ya Fedha, Kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi zake, kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha, Kamishina Msaidizi wa Idara ya Uendelezaj wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionensia Mjema (wa pili kushoto), Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa pili kulia), Mkoani kilimanjaro.
Katibu Tawala Mkoa Wa Kilimanjaro Bw. Yussuphu Nzowa, akizungumza na Timu ya Wataalam wa kutoa Elimu ya Fedha, Kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi zake, kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali Mkoani Kilimanjaro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Kilimanjaro)

About the author

mzalendoeditor