Dkt. Samia achagiza mapinduzi ya nishati Afrika
*Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia yajadiliwa kimataifa
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
Akizungumza leo Februari 12, 2025 jijini New Delhi, India katika Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi, Rwanda, Nepal, Brazili pamoja na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali kutoka India Dkt. Biteko amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha Nishati Safi ya Kupikia inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.
Mwaka 2022 Serikali ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ilisisitiza matumizi ya nishati safi na kueleza athari za matumizi ya nishati isiyokuwa safi kwa kuanzisha mjadala wa kwanza kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na faida zake kiuchimi na Kijamii.
Dkt. Biteko ametaja fursa mbalimbali za biashara ya Nishati Safi ya Kupikia nchini Tanzania, kama vile ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji, kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia.
Fursa zingine ni vituo vya kupokea LPG, vifaa vya uhifadhi, miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na maeneo jirani, usambazaji wa LNG wa kiwango kidogo, vifaa na mitungi ya gesi asilia.
“ Ningependa kuchukua fursa hii kuwataka wadau wote na wawekezaji katika sekta ya nishati kujiunga nasi katika malengo yetu makubwa lakini yanayoweza kufikiwa ya kupata umeme na nishati safi ya kupikia kuongeza sehemu ya nishati mbadala katika mchanganyiko wa nishati na kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi ili kusaidia upatikaji wa nishati,” amesema Dkt. Biteko.
ametaja jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia “Tanzania imekamilisha maendeleo ya Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa mwaka 2024-2034 wenye lengo kuu la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, ”
Ameongeza kuwa uzoefu unaonesha kuwa “ Katika kujifunza India imefanya vizuri katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2023, asilimia 71.1 ya watu wa India walikuwa wakitumia nishati safi ya kupikia. Hii imetokana na umuhimu wa kuhusisha sekta binafsi na kuunganishwa kwa ruzuku kwa kaya zenye kipato cha chini,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amesema takriban watu bilioni 2.3 duniani hawapati nishati safi ya kupikia na watu milioni 990 Kusini mwa Jangwa la Sahara hawajafikiwa matumizi na nishati safi. Hali hii inasababisha matatizo ya afya, uharibufu wa mazingira na matatizo ya kiuchumi,”
Vilevile, amesema Rais Samia amedhamiria kuinadi ajenda ya nishati safi ya kupikia nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika, ambapo katika mkutano wa COP 28, alizindua Programu ya Uwezeshaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake wa Afrika (AWCCSP), iliyoelekezwa kukabiliana na changamoto kubwa za kijinsia, mazingira, afya, na kiuchumi zinazowakabili wanawake na wasichana barani humo.
Akiendelea kuelezea msimamo wa Tanzania katika kuhamasisha Ajenda ya Matumizi ya Nishati Safi kimataifa, Dkt Biteko amesema mwaka 2024 Rais Samia alishiriki katika Mkutano wa Juu wa Nishati Safi ya Kupikia nchini Ufaransa ambapo alikuwa Mwenyekiti mwenza, na takriban dola bilioni 2.2 ziliahidiwa kwa ajili kusaidia ajenda hiyo barani Afrika.
Aidha, Tanzania kwa kushirikiana na Tume ya Nishati ya Afrika (AFREC) ilifanya Mkutano wa Kiwango cha Juu kuhusu Kupikia Safi barani Afrika katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 2024 pamoja na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliyofanyika jijini Dar es salaam Februari 27 na 28 mwaka huu kwa ajili ya kueleza dhamira zao kuhusu Mikataba ya Nishati ya Kitaifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh ametaja madhara ya matumizi ya nishati isiyosafi “ Kumekuwepo na idadi ya vifo takribani milioni 2, lakini wanawake na watoto wanapata madhara zaidi, huku wanawake wakitumia hadi saa 5 kila siku kwa ajili ya kutafuta kuni na kuandaa chakula,”
Akielezea mafanikio ya matumizi ya nishati safi nchini India, amesema sasa watu milioni 330 wameunganishwa na matumizi ya gesi au nishati safi.
“ Nishati safi sasa inapatikana kwa watu na maisha yamekuwa rahisi na shughuli zimeendelea kufanyika kwa ufanisi, sioni kwa nini hatuwezi kufanya hivi kwa kila mwananchi inawezekana.” Amemalizia Mhe. Signh
Kimsingi mkutano huo wa Mawaziri wa Nishati unatajwa kuwa muhimu katika jitihada za kuendeleza matumizi ya nishati safi duniani ambao umetoa fursa kwa mawaziri waliohudhuria kueleza jitihada zinazofanyika za kukuza matumizi ya nishati safi katika nchi zao.
Aidha, masuala ya sera, mila za watu, uhamasishaji, ubunifu, miundombinu ya usambazaji na wawekezaji yanatajwa kuwa mchango muhimu ya mafanikio ya matumizi ya nishati safi.